Nyie watu mmemsikia kocha wa Chelsea anavyojitapa lakini?

Tuesday October 9 2018

 

CHELSEA haijafungwa mechi yoyote kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Imeshinda mechi sita na kutoka sare mbili kwenye mechi nane ilizocheza, imekusanya pointi 20 na imekabana koo na Manchester City na Liverpool kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, ikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa tu.

Chelsea yenyewe imefunga mabao 18 hadi sasa.

Lakini, kwenye mabao yote hayo, Kocha Maurizio Sarri amekoshwa na bao moja tu, lilifungwa juzi Jumapili kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Southampton huko St Mary’s.

Sarri alikoshwa na bao la Alvaro Morata, ambalo lilikuwa la tatu katika mechi hiyo.

Straika huyo wa Kihispaniola alifunga bao hilo baada ya kupigwa pasi 31, kabla ya Morata kuweka mpira kwenye nyavu na Sarri, akasema: “Hili ndio soka langu.”

Kwenye mechi hiyo, Chelsea ilikuwa kwenye jezi tofauti kabisa, lakini jambo hilo halikuwa na utofauti kwa Eden Hazard kwani aliendelea tu kutupia, akifunga bao lake la saba msimu huu kwenye ligi hiyo, huku Ross Barkley naye akiwa na bahati na uzi huo mpya baada ya kutupia wavuni kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu kupita.

“Hivi ndivyo ninavyotaka timu yangu icheze,” alisema Sarri huku akitabasamu.

“Tuliuhamisha mpira kwa kasi sana, nadhani kugusa mpira mara moja au mbili inatosha. Ndio soka langu hili ninalotaka.”

Advertisement