Mikel naye kula pesa za Wachina

Saturday January 7 2017

KIUNGO John Mikel Obi ameamua kufuata mkumbo wa mastaa wanaokwenda kucheza soka lao China baada ya hivi karibuni kukamilisha uhamisho wa kujiunga na klabu ya Tianjin TEDA.

Mikel ameamua kutimkia China baada ya mambo kwenda kombo kwenye kikosi cha kwanza cha Chelsea, ambapo amekuwa akisugua benchi msimu huu tangu N’Golo Kante alipotua kwenye kikosi na Kocha Antonio Conte anawafikiria viungo wengine akiwamo Nemanja Matic, Nathaniel Chalobah na Cesc Fabregas. Staa huyo wa kimataifa wa Nigeria, Mikel ameelezwa kwamba kwenye klabu hiyo mpya atakuwa akipokea mshahara wa Pauni 140,000 kwa wiki.

Kwenye kikosi cha Chelsea alichojiunga nacho Julai 2006 kwa ada ya Pauni 17 milioni akitoka Lyn Oslo, kiungo huyo amecheza mechi 372 na kufunga mabao sita, huku akibeba ubingwa wa Ligi Kuu England mara mbili, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja, Europa League mara moja, Kombe la FA mara nne na Kombe la Ligi mara mbili.

Juzi, Alhamisi alifanyiwa vipimo vya afya, hivyo kuwa mchezaji wa pili wa Chelsea ndani ya siku chache tu kuondoka Stamford Bridge kwenda Mashariki ya Mbali baada ya kiungo Oscar kutimkia Shanghai SIPG.