Mchawi Manchester United atajwa hadharani

MANCHESTER, ENGLAND

KINACHOSEMWA huko Manchester United ni kwamba vipengele vilivyowekwa kwenye mikataba ya masupastaa Alexis Sanchez na Paul Pogba ndiyo uchawi unaochafua hali ya hewa katika timu hiyo na kumpa shughuli pevu kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Shida kubwa ni kuhusu vipengele vilivyowekwa kwenye mikataba ya wachezaji hao kwamba wanapokea bonasi kubwa ya kila bao wanalofunga au pasi ya bao wanayotoa huku wachezaji wengine mikataba yao hakuna kipengele kama hicho.

Ripoti zinadai kwamba, Sanchez ambaye analipwa Pauni 505,000 kwa wiki, kila akifunga basi anapata bonasi ya Pauni 75,000 na akitoa pasi ya bao basi analipwa Pauni 25,000. Kuhusu Pogba ni kwamba yeye akifunga bao, basi analipwa Pauni 50,000 na kama akipiga pasi ya bao, basi bonasi inayoingia kwenye akaunti yake ya benki ni Pauni 20,000. Kwa maana hiyo mabao na asisti alizopiga Pogba msimu huu zimemwingizia pesa za kutosha hapo ukiweka kando mshahara wake wa kila wiki.

Jambo hilo limedaiwa kutibua hali ya hewa huko Old Trafford kuhusu wachezaji wengine wakiamini nao wanastahili mikataba yao kuwekwa vipengele vya aina hiyo. Mpango huo ulitajwa kwamba ulianzishwa ili tu kupunguza ukubwa wa mishahara, kwamba bonasi ziwe nyingi kwa kila mchezaji, lakini ule mshahara wake kwa wiki uwe wa kiwango cha chini. Hata hivyo, suala la bonasi za mabao imeelezwa kuwa ni jambo la kawaida kwa klabu za Ulaya kwa miaka ya sasa, lakini ukubwa wa pesa wanazolipa Man United ndizo zinazoleta kasheshe kwa maana ya kuwatia wivu wengine.

Bao moja tu analofunga Sanchez kwenye kikosi cha Man United unalipa mishahara ya wiki ya wachezaji kibao kwenye Ligi Kuu England. Chanzo cha kutoka Old Trafford kilifichua kwamba hizo bonasi ndiyo tatizo kubwa kwenye kikosi cha Man United kwa sasa.