Mbappe ajikabidhi mapema Ballon d’Or

Muktasari:

  • Mastaa wa dunia, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo waliotwaa tuzo hizo mara tano kila mmoja, pia wamo japokuwa wengi wanaamini kipindi cha wachezaji hao kimeshamalizika.

PARIS, Ufaransa.MASTAA kibao wanaoujua mpira wao, wametulia wakisikilizia nani ataibuka mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or lakini mshambuliaji wa PSG na timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe amesema hiyo safari hii haambiwi kitu, ni yake.

Mbappe aliyekuwa katika kikosi cha Ufaransa kilichotwaa Kombe la Dunia 2018 akichangia pakubwa kutwaa ubingwa huo, alisema atajishangaa endapo ataikosa tuzo hiyo itakayotolewa Desemba 3.

Mchezaji huyo bora wa mwaka wa Ufaransa, ni kati ya wachezaji sita wa kikosi cha Didier Deschamps’ kilichokuwa Russia kwenye Fainali za Kombe la Dunia Russia 2018 waliotajwa kwenye tuzo hiyo.

Mastaa wa dunia, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo waliotwaa tuzo hizo mara tano kila mmoja, pia wamo japokuwa wengi wanaamini kipindi cha wachezaji hao kimeshamalizika.

Mshambuliaji wa Chelsea na Ubelgiji, Eden Hazard naye amekuwa akitajwatajwa kutokana na soka lake ya kiwango huku Luka Modric wa Real Madrid na Croatia naye pia anatajwa kutokana na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Fainali za Kombe la Dunia za Fifa.

Mbappe, anaamini anaweza kutwaa tuzo hiyo lakini anaweza kuikosa vilevile kutokana na ushindani wa wenzake.

“Ninatumai kila mshindi atafurahi na ni kwa sisi wa Kombe la Dunia. Najua nitakuwa mimi japokuwa nauona ushindani wa karibu zaidi.”