Manchester United kumkosa Sanchez leo

Muktasari:

  • Manchester United leo usiku itakuwa na kazi pevu ya kumzuia mshambuliaji mahiri wa Juventus, Cristiano Ronaldo asifunge wala asitengeneze mabao, timu hizo zitakapokutana kwenye Uwanja wa Old Trafford katika mchezo wa tatu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Manchester, England. Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho, atamkosa mshambuliaji wake mahiri Alexis Sanchez katika mchezo wa leo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Juventus.
Sanchez aliumia na kupumzishwa katika mchezo uliopita dhidi ya Chelsea, uliochezwa Jumamosi iliyopita na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2, ambapo Mourinho amesema anakosekana katika mchezo muhimu.
Mchezo huo wa leo utachezwa kwenye Uwanja wa Old Trafford na unaweza kuwa mbaya kwa Mourinho iwapo vijana wake watashindwa kumdhibiti mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo Cristiano Ronaldo anayeitumikia Juventus akitokea Real Madrid.
Mourinho alisema ingawa wanatamani kupata ushindi, lakini anakubaliana na ushauri wa matabibu wa klabu hiyo kutomtumia Sanchez aliyejitonesha kifundo cha Jumamosi iliyopita na nyota huyo anayelipwa mshahara mkubwa wa Pauni 500,000 kwa wiki, atakuwa nje kwa kipindi cha wiki mbili hadi tatu.
Mshambuliaji huyo alimkuna Mourinho alipofunga bao la ushindi walipoishinda Newcastle United kwa mabao 3-2 likiwa ni bao lake la kwanza tangu Aprili alipofungwa bao la ushindi katika nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Tottenham.
Akiuzungumzia mchezo huo wa Mourinho, alisema ni mtihani mkubwa kwake kwani mbali ya Sanchez pia atawakosa wachezaji wengine kadhaa ambao ni majeruhi.
Aliwataja baadhi ya wachezaji anaotarajia kuwakosa kuwa ni pamoja na Marouane Fellaini, Victor Lindelof, Diogo Dalot, Scott McTominay na mshambuliaji kinda wa Uingereza, Jesse Lingard.
Kukosekana kwao kwenye mazoezi ya timu hiyo kwenye uwanja wao wa Carrington jana Jumatatu kunamaanisha kuwa kocha huyo atawapanga Anthony Martial, Juan Mata na Marcus Rashford kumsaidia Romelu Lukaku katika safu ya ushambuliaji.
Man United iliyoanza ligi hiyo vizuri ikiishindilia Young Boys ya Uswisi kwa mabao 3-0 ikiwa ugenini ilibanwa na Valencia katika mechi yake ya pili na kulazimishwa sare ya 0-0 kwenye uwanja wa Old Trafford.
Mchezo wa leo ni mtihani mwingine kwa Mourinho, ikizingatiwa kuwa Juventus haijapoteza mechi yoyote msimu huu na katika Ligi Kuu Italia na ligi ya Mabingwa ilianza kwa kuichapa Valencia 2-0 ugenini kabla ya kuinyuka Young Boys 3-0.
Pengine sare ya mabao 2-2 iliyopiata Man United mbele ya Chelsea Jumamosi iliyopita itaipa nguvu ya kuondoka na ushindi leo mbele ya Juventus inayoongozwa na Ronaldo, mshambuliaji wa zamani ‘Mashetani wekundu hao’.