Kwa Jose, Perez uvamizi hatari

Tuesday November 20 2018

 

Madrid, Hispania.UKISIKIA uchokozi ndio huu, Real Madrid imevamia Ligi Kuu England ikiwa na kitita cha Pauni 320 milioni. Jamaa wanataka kufagia nyota wakali katika EPL bila aibu.

Taarifa zilizopatikana kutoka katika klabu hiyo zinasema uongozi wa Real Madrid umechoka kudhalilika katika ligi msimu huu na kwa sasa wanashika nafasi sita La Liga, wakiwa wamecheza mechi 12 na kupata pointi 20. Huu ni mwenendo mbaya katika siku za karibuni. Pengo la Cristiano Ronaldo aliyehamia Juventus linaonekana wazi na sasa wanataka kuliziba.

Kuna nyota kibao ambao wanawasaka katika Ligi Kuu England lakini majina ambayo yanapewa kipaumbele ni Christian Eriksen wa Tottenham, ambaye anapatikana kwa Euro 80 milioni Eden Hazard wa Chelsea ambaye anapatikana na kwa Euro 150 milioni na Marcus Rashford wa Manchester United ambaye ili kumpata unatakiwa kutoa Euro 60 milioni.

Pamoja na kuwa na orodha hiyo, Real Madrid wanaanza na kinda wa Fulham Ryan Sessegnon ambaye pia amekuwa akisakwa na Manchester United Liverpool na Tottenham.

Kocha wa Manchester United Jose Mourinho pia yupo katika mbio za kusaka saini ya mchezaji huyo na suala la Real kumsaka kwa udi na uvumba ni pigo kwake.

Mchezaji huyo ameonyesha soka la kutakata na sasa klabu hazitaki kufanya masihala katika kuwania saini yake.

Mchezaji huyo ni wa kikosi cha vijana cha England na makali yake aliyaonyesha wakati wa kuipandisha daraja Fulham na hivi karibuni alikiri klabu kadhaa zimekuwa zikimsaka ikiwa ni pamoja na Real Madrid.

“Unapotafutwa na klabu kadhaa unajisikia vizuri, lakini huwa najisemea moyoni, kazi yangu ni kucheza na wala si kusikiliza au kupata shauku ya mambo yanayoendelea. Kwa sasa naichezea Fulham ingawa huwezi kujua ya baadaye,” alisema mchezaji huyo ambaye ili umnase unatakiwa kutoa kiasi cha Pauni 30 milioni.

Taarifa kutoka Real zinasema ingawa wanahitaji wachezaji wakubwa na wenye uzoefu, wachezaji wadogo ndio watawapa kipaumbele, lengo ni kuwakuza na kuwaonyesha njia sahihi ya Real Madrid kwa miaka mingi.

Advertisement