Kumbe mchawi wa Zidane ni Bale

Muktasari:

  • Zidane ameondoka Madrid kwa sababu alitaka Bale auzwe, lakini Perez akabadili mawazo na kumtaka staa huyo wa Wales aendelee kubaki Bernabeu

MADRID, HISPANIA, WANASEMA hakuna msiba unaokosa sababu. Zinedine Zidane amewaachia msiba mkubwa huko Real Madrid na kinachoelezwa ni kwamba Mfaransa huyo aliamua kuachana na wababe hao wa Bernabeu, sababu ni Gareth Bale.
Taarifa za kutoka Hispania zinadai kwamba Zidane aliamua kuachana na Los Blancos baada ya kuvunjika kwa ahadi iliyokuwa imewekwa juu ya supastaa na mchezaji ghali wa kikosi hicho, Bale.
Zidane aliacha mshtuko mkubwa wakati alipoondoka kwenye kikosi hicho, ikiwa ni wiki chache tangu alipotoka kuwaongoza Los Blancos wakibeba taji lao la tatu mfululizo la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita. Katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool, Bale alifunga bao matata kabisa la tick-tack na hilo lilichochea zaidi tatizo lililopo baina ya Zidane na rais wa klabu hiyo, Florentino Perez.
Gazeti lenye heshima kubwa Hispania, El Pais lilidai kwamba bao lile la Bale lilimfanya Perez kuanza kufikiria upya mpango wa kumuuza mchezaji huyo, ambapo Zidane amekuwa akitaka iwe hivyo tangu msimu wa ligi ya ndani ya Hispania ulipokuwa umefika tamati.
Perez aliona ni vyema kubaki na Bale kuliko Cristiano Ronaldo na hilo linatajwa kwamba lilichangia kocha Zidane kufungasha virago vyake na kuondoka. Ronaldo pia aliuzwa kwenda Juventus, huku Bale akibakizwa kwenye timu hiyo licha ya hapo mwanzoni staa huyo wa Wales kuhusishwa sana na mpango wa kwenda Manchester United.
Kwa kifupi tu, Zidane na Bale hawakuwa na uhusiano mzuri sana, lakini msimamo wa Perez ulimfanya kocha huyo kufeli kwenye mipango yake na hivyo kuamua yeye kufungasha virago vyake na kuachana na maisha ya Bernabeu.
Mpango wa Zidane ulikuwa kumuuza Bale na pesa itakayopatikaba basi itumike kwenye kumnasa mmoja kati ya mastaa hawa, Mohamed Salah, Eden Hazard au Harry Kane. Mwanzoni Perez alikubaliana na mpango huo, lakini baada ya kufungwa kwa bao lile maridadi kabisa, rais huyo wa Bernabeu alibadili msimamo wake na akafuta mpango wa kumuuza Bale. Zidane alifahamu pia kwa mabao ya Bale aliyofunga kwenye fainali hiyo ni kama kumuumbua kocha huyo kwa sababu alimwaanzishia kwenye benchi. Zidane hakutaka kuendelea kuumbuliwa na Bale kwa muda mwingi zaidi na kuamua kuondoka zake. Mapema wiki hii ilibainisha kwamba Man United walikuwa na mpango wa kumbeba kocha huyo akarithi mikoba ya Jose Mourinho kabla ya mambo kupinduka na Mfaransa huy kwa sasa anahusishwa na Bayern Munich kwamba anaweza kwenda kumbadili Nico Kovac.
Hata hivyo, hali ya hewa bado haijatulia sana huko Man United licha ya ushindi wao wa Jumamosi iliyopita dhidi ya Newcastle na kama mambo yataendelea kuwa hovyo, basi mabosi wa huko Old Trafford wanaweza kugonga hodi kwa Zidane aje kunusuru hali ya mambo kwenye kikosi hicho. Mourinho aliiweka Man United kwenye matatizo makubwa baada ya kutibuana na karibu mastaa wake wote muhimu wa kikosi cha kwanza ikiwamo ugomvi wake wa hivi karibuni dhidi ya Alexis Sanchez. Kitu cha kufurahisha katika mechi hiyo ya ushindi dhidi ya Newcastle ambao uliokoa kibarua cha Mourinho, wachezaji wote ambao alitibuana nao, ndio waliofunga mabao. Juan Mata, Anthony Martial na Sanchez.
Jana Alhamisi, Mourinho alitarajia kukutana na makamu mwenyekiti wa Man United, Ed Woodward huko London na kama kutakuwa na makubaliano mazuri ya kocha huyo kuendelea kubaki na Mashetani Wekundu hao wa jijini Manchester basi ni wazi atawaambia wamsajilie nyota kadhaa hasa mabeki kwenye dirisha la Januari.

SUMMARY
Zidane ameondoka Madrid kwa sababu alitaka Bale auzwe, lakini Perez akabadili mawazo na kumtaka staa huyo wa Wales aendelee kubaki Bernabeu

.