Kane hataki sifa za kijinga

Sunday September 9 2018

 

STRAIKA, Harry Kane amekataa kulewa sifa za kijinga kutokana na kuwapo na watu wanaomlinganisha ubora na masupastaa wa nguvu duniani, Cristiano Ronaldo anayekipiga Juventus na Lionel Messi wa Barcelona.

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate hivi karibuni alimwelezea Kane ndiye Namba 9 bora zaidi duniani kwa sasa, lakini staa huyo wa Tottenham Hotspur ameibuka na kudai bado ana safari ndefu sana ya kuwafikia wababe Ronaldo na Messi.

Fowadi huyo ambaye alishinda tuzo ya Kiatu cha Dhahabu kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Russia, alisema bado kulinganishwa na wakali hao kwa sababu ni wachezaji wa daraja jingine kabisa, hajalifikia.

“Nadhani ni ngumu sana kujilinganisha na watu wale wawili, nilishasema hilo kwa sababu watu wale wameufanya mchezo wa soka kuwa wao kwa miaka 10 sasa,” alisema Kane.

“Sidhani kama nimefikia kiwango hicho. Ndivyo ninavyojiona na ndio maana nataka kujiongeza zaidi. Kwenye Kombe la Dunia mambo yalikuwa mazuri kwangu, lakini bado kuna mambo mengi ya kuyaboresha.”

Advertisement