Kalinic aliyetimulia Croatia aikataa medali

Muktasari:

Mshambuliaji huyo aliikataa medali hiyo aliyopewa wakati wa hafla ya kuwapongeza mashujaa hao wa Taifa waliofungwa mabao 4-2 na Ufaransa katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia.

Zagreb, Croatia. Mshambuliaji Nikola Kalinic, amekataa kupokea medali ya fedha waliyopewa wachezaji wa Croatia kwa kushika nafasi ya pili katika fainali za Kombe la Dunia 2018.
Mshambuliaji huyo aliikataa medali hiyo aliyopewa wakati wa hafla ya kuwapongeza mashujaa hao wa Taifa waliofungwa mabao 4-2 na Ufaransa katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia.
Kalinic, alitimuliwa kwenye kikosi cha Croatia baada ya kukataa kuingia uwanjani dakika ya 85 katika mechi waliyoishinda Nigeria mabao 2-0 siku ya pili baada ya ufunguzi wa fainali hizo.
Kutokana na kiburi alichokionyesha, Kocha Zlatko Dalic aliamua kumuondoa kwenye kikosi chake mshambuliaji huyo wa AC Milan ya Italia jambo lililoifanya Croatia kubakia na wachezaji 22 kwa muda wote wa fainali hizo.
“Ninashukuru sana kwa heshima hii niliyopewa lakini siwezi kuichukua medali hii kwa kuwa mimi sikucheza mechi yoyote kule Russia, hivyo sistahili kupata heshima hii,” alisema Kalinic.