Jezi ya Lionel Messi yamvuruga kinoma Romero

Sunday September 9 2018

 

KIPA wa Argentina, Sergio Romero amesema anashindwa kufahamu kwa nini jezi namba 10 ya timu hiyo iliyokuwa ikivaliwa na Lionel Messi haoni mtu anayeitumia katika mechi za kimataifa wanazocheza kwa sasa.

Jezi hiyo haitatumika na mchezaji yeyote katika mechi mbili za Argentina itakazocheza na Guatemala na Colombia kutokana na makubaliano yaliyofanywa kati ya kocha wa mpito Lionel Scaloni na chama cha soka cha Argentina.

Messi, ambaye hatima yake ya soka la kimataifa bado imekuwa kwenye sintofahamu, hayupo kwenye kikosi cha sasa cha Kocha Scaloni.

Lakini, kipa huyo wa Manchester United, Romero ameachwa na maswali mengi kutokana na jezi hiyo kushindwa kupewa mtu.

“Ile namba 10 imekuwa ikitumika kila wakati. Sijui kwa nini kwa sasa haitumiki. Sijauliza na wala sijaitaka, sijui tu kwa nini haitumiki,” alisema.

Advertisement