Hadi Lionel Messi kakubali mavitu ya Cristiano Ronaldo

Friday March 15 2019

 

BARCELONA, HISPANIA,

LIONEL Messi sio mtu wa roho mbaya baada ya kuchukua muda wake kumsifia Cristiano Ronaldo amefanya maajabu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kile alichoifanyia Atletico Madrid Jumanne iliyopita.

Staa huyo wa zamani wa Real Madrid, Ronaldo aliyekuwa mpinzani mkubwa wa Messi huko kwenye La Liga, aliibeba Juventus kwa mgongo wake na kuifikisha hatua ya robo fainali baada ya kupiga hat-trick na kupindua matokeo ya kipigo cha kwenye mechi ya mwanzo kutoka kwa Atletico.

Juve ikiburuzwa kwa mabao 2-0 kwenye mechi ya kwanza, Mreno huyo aliendeleza upinzani wake na Atletico, licha ya kwamba amehamia Italia baada ya kutikisa nyavu mara tatu na kuwafanya wababe hao wa Serie A kutinga kwenye nane bora ya michuano hiyo ya Ulaya. Messi mwenyewe alipiga mbili usiku wa juzi Jumatano wakati alipokiongoza kikosi chake cha Barcelona kikiichapa Lyon 5-1, lakini bado alimsifu mpinzani wake huyo wa zamani.

“Nadhani kile kichotokea kwa Ronaldo na Juventus ni matata kwelikweli. Nilidhani Atletico wangekuwa wagumu, lakini Juventus iliwabana na Cristiano alikuwa na usiku bora kabisa akifunga mara tatu,” alisema Messi.

Ronaldo alikuwa kwenye ubora wake katika mechi hiyo ambayo inamfanya kujiweka pazuri kwenye mchakamchaka wake wa kufukuzia taji lake la tano kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Messi na Ronaldo wanaweza kupangwa kumenyana kwenye hatua ya robo fainali ambapo droo yake inapangwa leo Ijumaa.

Advertisement