HUZUNI : Mane atukanwa na mashabiki Senegal,amwaga chozi

Muktasari:

 

  • Senegal imefuzu Afcon na sasa inaongoza katika kundi lake. Mpaka sasa Mane hajaifungia Senegal bao lolote huku Salah akiwa ameifungia Misri mabao manne katika mechi tatu na Ijumaa usiku alifunga bao la ushindi la dakika za majeruhi wakati Misri ikiichapa Tunisia 3-2.

DAKAR, SENEGAL.NABII hakubaliki kwao. Wakati mashabiki wa Liverpool wakikoshwa na kiwango cha staa wao wa kimataifa wa Senegal, Sadio Mane, hali ni tofauti kabisa nyumbani kwao.

Juzi staa huyo aliondoka uwanjani akilia baada ya kuzomewa kwa muda wote wa pambano dhidi ya Guinea ya Ikweta.

Senegal ilishinda bao moja, lakini kwa muda mwingi wa mchezo Mane alikuwa akizomewa na mashabiki wa nyumbani baada ya kukosa nafasi moja ya wazi katika lango la wapinzani wao na mwisho wa mechi wachezaji wenzake walilazimika kumbeba kumtoa nje ya uwanja baada ya staa huyo kuangua kilio.

Mane alifunika sura yake na jezi yake huku pia ikidaiwa moja kati ya sababu ya kilio chake ilikuwa ni kujutia kutofunga huku hasimu wake mkubwa katika soka la Afrika, Mohamed Salah ambaye ni staa mwenzake wa Liverpool akiwa katika nafasi nzuri ya kumpiku katika Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika pamoja na ile ya mfungaji bora.

Senegal imefuzu Afcon na sasa inaongoza katika kundi lake. Mpaka sasa Mane hajaifungia Senegal bao lolote huku Salah akiwa ameifungia Misri mabao manne katika mechi tatu na Ijumaa usiku alifunga bao la ushindi la dakika za majeruhi wakati Misri ikiichapa Tunisia 3-2.

Kaka yake Mane aliandika ujumbe mrefu kuelezea jinsi ambavyo staa huyo amekuwa hapewi sapoti na watu wa taifa lake tofauti na vile ambavyo mashabiki wa Misri wamekuwa wakimsapoti staa wao, Salah.

“Ni nadra kuona nchi ambayo haimpendi staa wake kama mnavyofanya. Misri yote inamsapoti Salah haijalishi kama anacheza vizuri au vibaya kwa timu ya taifa. Maelfu ya mashabiki wa Misri watamsapoti Salah lakini mashabiki wa Misri hawatamsapoti Kalidou Koulibaly (staa mwingine anayecheza Napoli) au Mane ambaye anawania tuzo ya Mwanasoka Bora na Salah. Ataendelea kupigana kwa ajili yenu, ataendelea kujitoa kafara na kutoa kila alichonacho kwa heshima na upendo wake kwa bendera ya taifa. Siku moja mtatambua lakini mnaweza kujikuta mmechelewa,” aliandika kaka huyo.

Mane na Salah wote wameanza kuwa katika fomu msimu huu huku wakiwa wamefunga mabao 15 kati yao. Wakati Mane akiwa amefunga mabao saba katika mechi 16, Salah amefunga mabao manane katika mechi 17.

Kumekuwa na hisia nyingi kutoka kwa mashabiki wa Afrika mastaa wao wamekuwa wakizitumikia zaidi klabu zao za Ulaya ambazo zinawalipa mishahara mikubwa kuliko wanavyozitumikia timu za mataifa yao.

Mara kadhaa wachezaji mastaa kutoka Ulaya wamekumbana na wakati mgumu pindi wanaposhindwa kung’ara katika mechi za timu zao za taifa huku wakiendelea kufunga kama kawaida pindi wanaporudi kucheza katika timu za Ulaya.

Staa wa zamani wa Ivory Coast, Didier Drogba naye aliwahi kuingia katika mkumbo huo, wakati nyota mwingine wa zamani wa Chelsea, Michael Essien naye aliwahi kushutumiwa kuikacha timu yake ya taifa mara kadhaa kwa kisingizio cha kuwa majeruhi lakini alikuwa anatesa katika kikosi cha Chelsea.

Kwa mara ya kwanza michuano ya Afcon itafanyika Juni tofauti na ambavyo ilikuwa ikifanyika Januari kwa mara nyingi.

Klabu za Ulaya hazitawakosa mastaa wao kama ambavyo zimekuwa zikiwakosa pindi michuano hiyo ilipokuwa ikifanyika Januari hadi Februari.