Dybala mwili upo Juve, moyo upo Madrid

Monday September 10 2018

 

STAA wa Juventus, Paulo Dybala ameripotiwa kutamani sana kujiunga na Real Madrid kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi kama sio Januari.

Dybala ametua Juventus akitokea Palmero kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka 2015 na staa huyo wa Kiargentina amefunga mabao 68 katika mechi 142 za michuano tofauti alizochezea mabingwa hao wa Italia.

Msimu uliopita ulionekana kuwa mzuri kwa Dybala kwa upande wa mabao aliyokuwa akifunga, ambapo aliweka kwenye nyavu mara 26 katika mechi 46 za michuano tofauti alizocheza, huku mabao 22 akifunga kwenye Serie A.

Dybala bado hajafunga kwenye ligi msimu huu, huku kukiwa na ripoti mambo yake hayajatulia baada ya kuwasili wa supastaa Cristiano Ronaldo kwenye kikosi hicho cha Turin.

Kwa mujibu wa Don Balon, fowadi huyo mwenye umri wa miaka 24 kwa sasa anachokiwaza ni kutua tu Bernabeu, hasa ukizingatia Los Blancos bado hawajapata mtu wa kuziba pengo la Ronaldo. Madrid imeanza msimu mpya ikishinda mechi zote tatu ilizocheza kwenye La Liga msimu huu.

Advertisement