DALOT Mreno atakayesaka namba aya Valencia

Saturday June 9 2018

 

MANCHESTER, ENGLAND. JOSE Mourinho, kocha wa Manchester United ameanza kukisuka upya kikosi chake cha Old Trafford akijaribu kuondoa aibu ya kutoka kapa msimu uliopita.

Ameanza kwa kumnasa kiungo wa Brazil, Fred kutoka Shakhtar lakini jicho lake la pili limeangukia kwa kinda wa nchini kwake Ureno, Diogo Dalot. Kwanini ametua kwa kinda huyo mwenye miaka 19. Ana siri gani Diogo?

Jina lake kamili ni José Diogo Dalot Teixeira na alizaliwa mnamo Machi 18, 1999 katika jiji la Braga nchini Ureno. Dalot alianza kucheza soka na kujiunga na timu ya watoto ya Porto ya Ureno akiwa na miaka tisa tu mnamo mwaka 2008.

Kabla ya hapo, klabu zote mbili kubwa za Ureno Porto na Benfica zilionyesha nia ya kumnasa lakini umbali wa kutoka kwao Braga kwenda Lisbon ulikuwa kikwazo. Hata hivyo baadaye ilionekana kuwa ingekuwa bora kama angetua Porto ambayo pia alikuwa akiishabikia utotoni.

Baada ya kuonyesha umahiri wake kwa muda mrefu hatimaye alitua katika timu B ya Porto na kucheza mechi yake ya kwanza katika pambano la daraja la kwanza dhidi ya Leixoes huku akicheza dakika zote tisini ingawa walichapwa mabao 2-1.

Kutokana na kiwango chake kuendelea kuimarika, Dalot alijikuta akicheza mechi yake ya kwanza katika kikosi cha wakubwa mnamo Oktoba 13, 2017 akianza katika pambano dhidi ya Lusitano G.C ambao walishinda mabao 6-0. Hili lilikuwa pambano la kombe la Ureno.

Alicheza mechi yake ya kwanza Ligi Kuu ya Ureno katika pambano dhidi ya Rio Ave mnamo Februari 18, 2018 akiingia katika dakika ya 75 na walishinda mabao 5-0. Pambano hili lilipigwa ugenini. Pambano lake la kwanza nyumbani katika dimba la Dragao lilikuja dhidi ya wapinzani wao wa jadi Sporting Lisbon. Dalot hakuonyesha wasiwasi wowote na alionyesha kiwango cha juu katika mechi hiyo na kusifiwa vilivyo huku Porto wakishinda mabao 2-1. Mechi hiyo iliifungulia Porto nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.

Katika pambano dhidi ya NOS ambalo Porto walishinda mabao 5-1, Dalot alipika mabao mawili na mwisho wa mchezo, kocha wa Porto, Sergio Conceicao ambaye ni staa wa zamani wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno alijikuta akimwamgia sifa kinda huyo.

“NI kijana ambaye amefanya kazi ya kipekee katika timu B. Dalot ana tabia njema lakini ni mapema. Mafanikio hayatokani tu na kiwango kizuri ambacho mtu ameonyesha, bali muendelezo wa ubora na pia kujiingiza zaidi katika kikosi cha Porto. Ana ubora wa kufanya hivyo. Ni mchezaji mzuri sana.” alisema Mechi pekee ya Ligi ya mabingwa wa Ulaya alicheza katika pambano dhidi ya Liverpool Machi 6 mwaka huu akicheza dakika zote 90 katika mechi ambayo ilimalizika kwa suluhu ya bila kufungana. Hata hivyo katika pambano la awali Porto walikuwa wamechapwa 5-0.

Mourinho amnasa, apagawa naye

Maskauti wa Manchester United nchini Ureno walifanikiwa kuona kipaji cha Dalot na kumfahamisha kocha wa Manchester United, Jose Mourinho ambaye ni raia mwenzake wa Ureno. Mourinho hakusita kumchukua kinda huyo ambaye sasa anataka kumpa changamoto mlinzi wake mkongwe, Antonio Valencia.

Juni 6 mwaka huu Dalot alisaini kuichezea Manchester United kwa dau la pauni 19 milioni. Alisaini mkataba wa miaka mitano ambao ulimfurahisha kocha, Jose Mourinho aliyemmwagia sifa mno kinda huyo staa.

“Diogo ni kinda mwenye kipaji kikubwa sana na sifa zote ambazo zitamfanya awe mchezaji mkubwa kwa klabu hii. Ana sifa zote ambazo mlinzi wa kulia anahitaji. Ana nguvu, mbinu, akili, huku pia akiwa amejengwa kwa misingi ya shule ya soka ya Porto ambayo inawaandaa

“Katika kundi la umri wake, yeye ndiye beki bora wa kulia na tunaamini kwamba ana muda wa kufanya makubwa katika siku za usoni Manchester United.”

Atesa timu za vijana Ureno

Dalot bado hajagusa jezi ya wakubwa ya timu ya taifa ya Ureno ingawa anatazamiwa kuitwa muda si mrefu baada ya kusaini kuichezea Manchester United hasa kama akifanikiwa kupata nafasi katika mechi mbalimbali msimu ujao.

Tayari ameshatamba katika timu za vijana chini ya umri wa miaka 17 na ile ya chini ya umri wa miaka 20. Alikisaidia kikosi cha Ureno chini ya umri wa miaka 17 mnamo mwaka 2016 katika Michuano ya Euro ya umri huo ambapo Ureno walitwaa taji hilo. Alifunga mabao mawili katika mechi tano za michuano hiyo iliyofanyika Azerbaijan na bao moja alifunga katika pambano la fainali dhidi ya Hispania. Mwaka huo huo alikuwa katika kikosi cha umri chini ya miaka 19 ambacho kilifika katika robo fainali za Euro chini ya umri wa miaka 10.

Dalot aliiwakilisha Ureno katika kikosi cha chini ya umri wa miaka 20 kombe la dunia akianza mechi zote kabla ya kutolewa hatua ya robo fainali.

Advertisement