Carragher, amshauri Rashford ahame Man United

Muktasari:

Jamie Carragher, beki wa zamani wa Liverpool ambaye kwa sasa ni mchambuzi mahiri wa soka England amedai kipaji cha Rashford kitakwenda juu zaidi na kuwa mchezaji mwenye ubora wa dunia kama akiondoka kwanza United halafu akarudi baadaye.

NI Ushauri au fitina dhidi ya Manchester United? Ni chungu kumeza lakini mmoja wa mastaa wa zamani wa soka amemshauri mshambuliaji mahiri wa Manchester United, Marcus Rashford kuondoka klabuni hapo kwa ajili ya kuwa mchezaji bora zaidi.

Jamie Carragher, beki wa zamani wa Liverpool ambaye kwa sasa ni mchambuzi mahiri wa soka England amedai kipaji cha Rashford kitakwenda juu zaidi na kuwa mchezaji mwenye ubora wa dunia kama akiondoka kwanza United halafu akarudi baadaye.

Rashford, 20, alifunga bao la ushindi katika pambano dhidi ya Uswisi juzi usiku likiwa ni bao lake la pili ndani ya mechi mbili baada ya kufunga bao jingine katika pambano la Jumamosi usiku dhidi ya Hispania wakichapwa mabao 2-1.

Hata hivyo, licha ya mabao hayo bado kuna uwezekano mkubwa Rashford akasugua benchi katika pambano la wikiendi hii dhidi ya Watford ugenini huku Kocha Jose Mourinho akitazamiwa kumchagua Romelu Lukaku kuongoza mashambulizi.

Carragher anaamini kwa sasa itakuwa ngumu kwa Rashford kuchukua nafasi ya Lukaku na badala yake anahitajika kwenda katika klabu kama Everton na kufunga mabao zaidi kama Lukaku alivyofanya ili arudi timu kubwa akiwa na makali.

“Simuoni Rashford akichukua nafasi ya Lukaku kama Lukaku akiendelea kuwa pale. Lakini Lukaku alikuwa Chelsea na amefanya kazi ngumu kuwa alipo ikiwamo kuondoka kwenda Everton. Aliishia kuwa mfungaji bora na alipata uhamisho wa kwenda Manchester United,” alisema Carragher.

“Everton ni klabu ambayo mtu kama Rashford anajua anaweza kucheza kila wiki. Msimu uliopita, alicheza ovyo mechi dhidi ya Brighton, Mourinho alimshambulia na mechi iliyofuata moja kwa moja Lukaku alikwenda kuanza mechi iliyofuata. Hilo ndio tatizo ambalo daima atakuwa nalo.”

Lukaku alinunuliwa kwa dau la Pauni 75 milioni akitokea Everton katika dirisha kubwa lililopita la majira joto akiwa amekamilisha mzunguko wake wa klabu mbalimbali baada ya kushindwa kung’ara akiwa na Chelsea iiyomleta England kutoka kwao Ubelgiji alikokuwa akichezea Anderlecht.

Staa huyo wa kimataifa wa Ubelgiji ambaye juzi alifunga mabao matatu dhidi ya Iceland katika mechi ya kimataifa, amewahi kucheza kwa mkopo katika klabu za West Brom na Everton kabla ya Everton kuamua kumchukua jumla na alipewa nafasi ya kucheza mara kwa mara na kutamba kwa kufunga mabao.

Carragher anaamini Rashford inabidi atiwe moyo na njia aliyotumia Lukaku kuwa staa mkubwa zaidi kwa sasa huku akiamini kuondoka katika moja kati ya klabu kubwa katika Ligi Kuu ya England inaweza kuwa jawabu.

“Nadhani iwe hivyo. Inafikia wakati unajiuliza kama anaweza kuwa mchezaji wa kati wa kudumu Manchester United au England huku akiwa kama mshambuliaji wa kati. Katika nafasi ile inabidi uwe na kiwango cha dunia. Rashford bado hajafika huko lakini anaweza kufika akiwa na miaka 24. Lukaku kwa sasa anaonekana kuwa mmoja kati ya washambuliaji bora duniani kwahiyo inawezekana Rashford ikabidi ahame na kurudi katika moja kati ya timu kubwa,” alimalizia Carragher

Endapo Rashford atafuata ushauru wa Carragher, basi timu nyingine yoyote atakayochezea itakuwa klabu ya kwanza nje ya Manchester United kuichezea. Aliingia katika shule ya soka ya United akiwa na umri wa miaka saba.

Aliingia katika kikosi cha United kwa mara ya kwanza Novemba 21, 2015 katika utawala wa Kocha Louis van Gaal lakini akaishia kukaa benchi katika pambano dhidi ya Watford huku wakishinda 2-1. Alicheza mechi yake ya kwanza katika pambano dhidi ya Midtjylland michuano ya Europa baada ya Anthony Martial kuumia. alifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 5-1.

Mabao hayo yalimfanya awe mfungaji kinda zaidi wa United katika michuano ya Ulaya akiipiku rekodi ya George Best. Alicheza mechi yake ya kwanza ya ligi siku tatu zilizofuata dhidi ya Arsenal na kufunga mabao mawili huku akipika moja katika ushindi wa mabao 3-2.

Kwa kufunga mabao hayo aliingia katika rekodi ya kuwa mchezaji wa tatu kinda zaidi kuifungia United katika ligi baada ya Federico Macheda na Danny Welbeck. Machi 20, 2016 alifunga bao katika pambano la watani wa jadi dhidi ya Manchester City ukiwa ni ushindi wa kwanza ugenini kwa watani hao tangu mwaka 2012. Kwa kufanya hivyo aliweka rekodi ya kuwa mfungaji mdogo zaidi wa pambano hilo la watani wa jadi akifanya hivyo akiwa na miaka 18 na siku 141.