Cantona amchana Mourinho, amtaka Pep Guardiola

Muktasari:

  • Cantona, mkongwe anayeheshimika Old Trafford ambaye aliingia klabuni hapo mwaka 1992 akitokea Leeds United na kuondoka mwaka 1997 huku akistaafu soka amedai kwamba Mourinho sio kocha sahihi wa United.

UPINZANI bado mkali kwa kocha, Jose Mourinho. anapokea mashambulizi kutoka kila mahala na sasa gwiji wa zamani wa Manchester United, Eric Cantona amejitokeza kumpiga fitina kocha huyo Mreno aliyekalia kuti kavu.

Cantona, mkongwe anayeheshimika Old Trafford ambaye aliingia klabuni hapo mwaka 1992 akitokea Leeds United na kuondoka mwaka 1997 huku akistaafu soka amedai kwamba Mourinho sio kocha sahihi wa United.

Badala yake, staa huyo wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa ameshindilia msumari wa moto katika kidonda kwa kudai kwamba kocha hasimu wa Mourinho, Pep Guardiola anayefundisha wapinzani wao Manchester City ndiye ambaye anastahili kukalia kiti cha Mourinho pale Old Trafford.

United imepoteza mechi mbili kati ya nne walizocheza mpaka sasa na cantona anaamini kwamba wanaweza kushinda mataji lakini chaguo lake kubwa ni Guardiola kuliko Mourinho.

“Mambo sio mazuri. Lakini ni mapema katika msimu. Ni mapema kusema lolote. Manchester United ni klabu kubwa na siku zote itakuwa kubwa. Watashinda mataji, najua watashinda mataji. Lakini wanachezaje? Sio vizuri sana. kocha amewafanya wacheze tofauti na mashabiki wanavyotaka. Haifurahishi na hakuna ubunifu. Nampenda Mourinho. ana hadhi nzuri lakini sio kocha sahihi kwa United. Ilibidi wamchukue Pep Guardiola,” alisema Cantona.

“(Pep) ilibidi awe pale, lakini anafanya kazi nzuri na klabu nyingine ambayo siiwezi kuitaja jina. Inaniuma sana. Manchester City. Inabidi niseme tu kwa sababu siwezi kujizuia. Naongea utani kwa Manchester City lakini wanacheza soka safi sana.

“Nafikiria tu kwamba Guardiola alipaswa kuwa United. Ana mzimu wa Johan Cruyff (kocha wa zamani wa Barcelona). Aliwahi kucheza chini ya Cruyff pale Barcelona na alijifunza kila kitu kutoka kwake. Pep ndiye mtu pekee ambaye alitakiwa kuwa United kwa sasa,” alisisitiza Cantona.

Cantona ambaye baada ya kuachana na United alijitumbukiza katika filamu amedai kwamba angependa kuifundisha Manchesteer United siku moja na endapo atapewa kibarua hicho timu hiyo itacheza soka la kuvutia.

“Ningependa kufundisha. Kama wakinipigia simu, nitakwenda, nitafurahia kazi. Wanajua nilipo. Baada ya hapo tutacheza soka la kuvutia tena. Nitakuwa mtu mzuri kwa mashabiki kama Alex Ferguson.

“Aliwaruhusu wachezaji wawe wabunifu. Aliwataka waonyeshe uwezo wao binafsi. Wote tulijiona watu wa maana sana kwake. Siku zote alikuwa anatusifu. Mtu mzuri, kiongozi mzuri,” alisema Cantona.

Huu unakuwa mfululizo wa mastaa wa zamani wa United kumshambulia Mourinho huku pia wakikisifu kiwango cha kocha wa timu yao pinzani Manchester City, Pep Guardiola.

Julai mwaka huu staa mwingine wa zamani wa Manchester United, Paul Scholes ambaye alicheza sambamba na Cantona enzi zake alidai kwamba United imekuwa haichezi mchezo wa kuvutia chini ya Mourinho huku akidokeza kwa hali isingekuwa hivyo kama kocha angekuwa Guardiola.

“Haonekani kuwa na furaha, lakini labda ana furaha. Labda wakati mwingine ni timu ambayo inapata matokeo kuliko kufurahisha ndio anayoitaka. Nadhani ndio maana ana furaha. Amekuwa hivyo kwa miaka mingi.”

“Kitu muhimu kwa Mourinho nadhani ni matokeo. Atahukumiwa kwa matokeo. Mwaka jana ulikuwa mwaka mbaya. Hakukuwa na haki yoyote ya kuchukua taji lakini jinsi walivyocheza katika ligi haikuwa katika kiwango kilichotakiwa. Kila mwaka ambao United hawashindi kitu inakuwa majanga na lawama zinakufuata mpaka ushinde ligi.”

Scholes aliweka wazi kwamba ingekuwa tofauti kama Guardiola angekuwa kocha wa United huku akisema: “Endapo Guardiola angekuwa kocha wa Manchester United angechukia kwa ambacho angekiona na mambo yangekuwa tofauti.”