‘Bila Ronaldo! Tutapata tabu sana’

Tuesday August 7 2018

 

KAMA unadhani mastaa wa Real Madrid wamefurahishwa na hatua ya mabosi zao kumuuza Cristiano Ronaldo, basi utakuwa unajidanganya sana na Toni Kroos ameamua kufunguka.

Kiungo huyo wa Kijerumani amefichua kuwa, kuondoka kwa Ronaldo kumeacha pengo kubwa na watapata sana kupata mtu wa kuziba nafasi yake hasa katika kupasia nyavuni.

Ronaldo, ambaye ni mshindi wa Ballon d’Or mara tano, ameachana na Madrid na kutua zake Juventus kwa dau la Euro 112 milioni huku akiibeba Los Blancos kubeba mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kroos amesema, haitakuwa shida kuanza msimu mpya bila Ronaldo, lakini kwenye kupachika mabao itakuwa suala gumu kwani, Mreno huyo alikuwa fundi na data zake zimekuwa juu muda wote.

“Mabao 50 kwa msimu sio kitu kidogo kabisa, Ronaldo ameifanya kazi yake vizuri na itakuwa vigumu sana kupata mtu wa kuifikia rekodi yake,” alisema Kroos.

“Cristiano alikuwa mtu muhimu katika timu kwa miaka kadhaa sasa, uwepo wake umetufanya bora uwanjani na kushinda mataji, lakini tutapata tabu sana hasa tukikutana na Juventus msimu huu katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.”

Advertisement