Bellerin amponda Arsene Wenger baada ya kuondoka

Sunday September 9 2018

HECTOR Bellerin yupo Arsenal kwa sasa kwa sababu Arsene Wenger ametaka iwe hivyo. Kuna wakati alitaka kuhama, lakini kocha huyo Mfaransa akamtuliza na kumpa maisha Emirates.

Hata hivyo, sasa kufumba na kufumbua, beki huyo Mhispaniola anaibuka na kumponda mtu aliyemfanya avae jezi za Washika Bunduki hao London, Wenger, hana mipango.

Bellerin akafika mbali zaidi akidai kwa sasa baada ya Arsenal kuwa chini ya Kocha mpya, Unai Emery anajiona kama yupo kwenye klabu mpya. Mhispaniola huyo amemponda Wenger kutokana na namna alivyokuwa akizichukulia mechi.

Arsenal imechapwa mechi mbili za mwanzo kwenye Ligi Kuu England msimu huu dhidi ya Manchester City na Chelsea, kabla ya kushinda mbili zilizofuatia, West Ham United na Cardiff City.

Licha ya mwanzo huo mgumu, beki huyo wa pembeni alisema Arsenal ipo kwenye mikono salama kwa sasa chini ya Emery, ambaye ni Mhispaniola mwenzake.

Bellerin alisema: “Najiona kama nipo kwenye klabu mpya.

“Tumekuwa na mambo mengi mapya. Ni aibu kubwa kwa wale walioondoka na ninafurahia mambo yote mapya.”

Bellerin alimsema Wenger akidai kwamba Arsenal ilikuwa inacheza soka lilelile dhidi ya kila mpinzani huku wakitarajia kushinda. “Kuna wachezaji wapo hapa kwa muda mrefu. Lakini, sasa watakuwa wanaelewa mambo haya mapya,” alisema.

“Nafurahishwa sana na Emery. Tulipoteza mechi mbili za kwanza, lakini hakuwa wabaya sana uwanjani. Baada ya zile mechi, wachezaji wenyewe waliona kuna kitu kinakuja na mambo yatakuwa sawa.

“Wenger alitaka tucheze staili ileile bila ya kujali mpinzani. Alichokuwa akitaka tucheze kama anavyotaka tucheze kila siku, huku akitaka tushinde. Hata hivyo, Emery ni mtu wa mipango, anaandaa timu yake kutokana na mpinzani.

Ni mtu makini sana. Miezi michache baadaye, naamini tutakuwa wazuri sana, tutafikia kwenye vile viwango vya juu tunavyovihitaji.”

Arsenal wanaamini wataendelea na makali yao kwenye Ligi Kuu England baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa ambapo sasa wataifuata Newcastle United huko kwao uwanjani St James’ Park.

Advertisement