Bao la Martial lazoa mamilioni Man United

Friday October 12 2018

 

MANCHESTER, ENGLAND, USHINDI wa kibabe wa Manchester United dhidi ya Newcastle United umeokoa kibarua cha Jose Mourinho, lakini imeripotiwa kwamba umeigharimu timu hiyo mamilioni ya pesa.
Kwenye mechi hiyo, Man United walikuwa nyuma kwa mabao 2-0 hadi mapumziko, lakini walitumia dakika 20 za mwisho, kufunga mabao matatu na kuibuka na ushindi wa 3-2 katika mechi ya Ligi Kuu England iliyofanyika uwanjani Old Trafford.
Baada ya Juan Mata kufunga bao la kwanza, Anthony Martial akaja kufunga la kusawazisha kabla ya Alexis Sanchez kufunnga la ushindi na kuwafanya kutuliza presha iliyokuwapo huko Old Trafford ambayo ilikuwa ikitishia usalama wa kibarua cha kocha wao Mourinho.
Lakini, lile bao alilofunga Martial limewagharimu Man United Pauni 7.7milioni. Unajua kwanini kwenye mkataba wa mchezaji huyo kuna kipengele kinachoeleza kwamba Man United watakuwa wakilipa pesa tu huko Monaco kwa kipindi cha miaka mitatu kama Martial atafikisha idadi fulani ya mabao.
Wakati Man United wanamnasa Martial walilipa Pauni 38.5 milioni, lakini kwenye makubaliano na vipengele vilivyowekwa kwenye mkataba wake, unaonyesha kwamba winga huyo wa Kifaransa atawagharimu wababe hao wa Englandn hadi Pauni 61.6 milioni. Moja ya makubaliano yaliyopo kwenye vipengele hivyo ni kwamba Man United watawalipa Monaco Pauni7.7 milioni kama Martial atafikisha mabao 25 kwenye Ligi Kuu England kabla ya msimu wa 2018-19 kufika mwisho. Januari mwaka huu kwenye mechi dhidi ya Burnley, Martial alifunga bao lake la 24 kwenye Ligi Kuu England, hivyo Monaco walikuwa wakisubiri bao moja tu wavute mkwanja huo matata. Subira hiyo imefika mwisho baada ya miezi 10 na hivyo, Martial alipofunga tu kwenye mechi ya Newcastle, basi hapo akaunti ya benki ya Monaco ikawa imetuna. Kwa kiasi hicho cha pesa, Man United sasa watakuwa wamemlipia Martial hadi Pauni 46.2 milioni hadi sasa.

Advertisement