Bale kachokwa jamani Madrid

Muktasari:

Mashabiki wa Los Blancos wanaonekana kumchoka Bale baada ya asilimia nane tu kati ya 400,000 ndio waliopiga kura kumtaka supastaa huyo wa kimataifa wa Wales aendelee kubaki kwenye timu hiyo msimu ujao, ikiwa na maana asilimia 92 wanataka auzwe.

MADRID, HISPANIA,

MASHABIKI wa Real Madrid wanaamini kocha wao, Zinedine Zidane atampiga bei Gareth Bale huku wakiwa na imani kubwa atanunuliwa Eden Hazard kuja kuziba pengo lake.

Hicho ndicho kinachoonekana kwenda kutokea.

Mashabiki wa Los Blancos wanaonekana kumchoka Bale baada ya asilimia nane tu kati ya 400,000 ndio waliopiga kura kumtaka supastaa huyo wa kimataifa wa Wales aendelee kubaki kwenye timu hiyo msimu ujao, ikiwa na maana asilimia 92 wanataka auzwe.

Kwenye mchakato huo, asilimia 53 ya mashabiki hao walitoa pendekezo la kusajiliwa Hazard kuziba pengo lake huko Bernabeu.

Kwa muda sasa Real Madrid wamekuwa wakihusishwa na mpango wa kumsajili Hazard anayetajwa na timu yake ya Chelsea thamani yake ni Pauni 100 milioni.

Mashabiki hao pia wamepiga kura ya kuwa na imani na Kocha Zidane katika kukinoa kikosi chao baada ya mambo kwenda kombo kwa sasa wakiwa hawana uhakika wa kubeba taji lolote kwa msimu huu.

Asilimia 47 ya mashabiki hao walisema wanaamini Bale atakuwa mchezaji atakayeathirika kwa kiwango kikubwa na kurejea kwa Kocha Zidane huku mchezaji mwenyewe akihusishwa na mpango wa kurudi kwenye Ligi Kuu England, ambako Manchester United inatajwa kusaka huduma yake.

Bale alisema: “Nataka kucheza kila wiki na hilo halionekana kutokea hapa msimu huu na hata msimu mwingine ujao. Itabidi niketi kitako mwishoni mwa msimu na kujadili mpango wangu baada ya hapo.”

Kwenye kura zilizopigwa, beki wa kulia Dani Carvajal ameongoza kwenye maoni ya mastaa wanaotakiwa abaki, akipata kura asilimia 94, huku wachezaji wengine wanaofuatia ni Mbrazili Vinicius na beki wa kushoto Mhispaniola, Sergio Reguilon. Wachezaji wengine waliopigwa kura za kubaki ni Raphael Varane, Keylor Navas na Luka Modric na Mhispaniola Isco.