Giannis na kaka yake kukinukisha Bucks

USAJILI unaendelea kama kawa kunako maandalizi ya ligi kubwa ya kikapu Marekani (NBA) kuelekea msimu mpya ujao baadaye mwaka huu ambapo kila timu imeendelea kuongeza na kutoa wacheaji ili kuimarisha vikosi kwa lengo la kufanya msimu uwe bora kwao.

Wiki hii kuna dili jipya limefanyika pale Milwaukee Bucks ambayo imemtoa kaka yake Giannis Antetokounmpo aitwaye Thanasis Antetokounmpo kutokea kwao Ugiriki barani Ulaya na wamemuunganisha naye kucheza pamoja msimu ujao.

Akiwa mchezaji huru baada ya kumalizika kwa mkataba wake na timu ya ligi ya kikapu nchini kwao Ugiriki ya Panathinaikos aliyoitumikia kwa misimu miwili iliyopita, Thanasis anatua Bucks akiwa ameiwezesha timu hiyo ya Ugiriki kushinda mataji mawili ya ligi ya nchini humo.

Kabla ya kurejea kwao Ugiriki,awali alikuwa mchezaji wa New York Knicks msimu wa 2015-2016 baada ya kutwaliwa na timu hiyo kwenye draft katika mchujo wa mwaka 2014 akitokea kucheza timu ya Delaware 87ers.

Meneja mkuu wa Milwaukee Bucks,Jon Horst akimtangaza mchezaji huyo alimtaja kama mchezaji atakayeongeza nguvu kwenye timu hiyo kulingana na alichokitaja kuwa mzoefu na mwenye uwezo wa kushindana hivyo wanatarajia kupata mazuri kutoka kwake akiwa sambamba na ndugu yake Giannis ambaye ni MVP wa msimu uliopita.