Jezi namba 23 ya LeBron yapigwa stop

KAMA ulikuwa hujui, jezi namba 23 ndio iliwatambulisha mastaa wawili wa Ligi ya Mpira wa Kikapu Marekani (NBA), LeBron James na Anthony Davis (AD) tangu waanze kucheza ligi hiyo.

LeBron alianza kuivaa jezi hiyo Clevaland Cavaliers mwaka 2003 kabla ya kusepa kama mchezaji huru mwaka 2010 kimaajabu baada ya kushindwa kubeba taji akiwa na timu hiyo.

Alitua Miami Heat mahali ambako alipofanikiwa kubeba taji hilo mara mbili akiwa na jezi mpya namba sita kabla ya kurudi tena Cavaliers mwaka 2014 na kurejea katika jezi yake namba yake 23.

Msimu uliopita LeBron alianza kuichezea timu yake mpya ya Los Angeles Lakers na kuendelea kuitumikia jezi namba 23 kabla ya kuamua kuiacha na kurudia namba sita.

Lengo la kuachana na jezi hiyo lilikuwa ni kumwachia nyota Anthony Davis aliyesaini kutokea New Orleans Pelicans ambaye tangu aanze kucheza ligi hiyo hajawahi kuvaa namba nyingine zaidi ya 23.

Hata hivyo, pamoja na nia nzuri aliyoionyesha LeBron kwa AD, balaa limezuka baada ya Kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike kuweka ngumu.

Nike ambao ndio wenye haki za mauzo za jezi za nyota huyo wamepinga mpango huo wakihofia hasara kwa kuwa tayari wameshatengeneza jezi za LeBron zenye namba 23 ikiwa na maana ililenga kuziweka sokoni kwa ajili ya mashabiki wa nyota huyo.

Kutokana na ngumu hiyo ya Nike, sasa LeBron ataendelea kuvalia jezi namba 23, huku AD akitumia namba tatu na tayari utambulisho wa jezi hizo umewekwa wazi.