Arsenal yatikisa EPL

Tuesday October 9 2018

 

MNAMJUA Unai Emery? Kama humjui, basi ndiye kocha mpya wa Arsenal hii, ambayo yenyewe inachapachapa tu.

Wakati wakiwa wameshinda mechi tisa mfululizo hadi sasa, lakini Emery amesema kikosi chake bado kipo kwenye mabadiliko ya taratibu, hakijafikia pale anapopahitaji. Nakwambia mtakoma.

Emery alisema: “Sidhani kama tupo vizuri sana, tutakuwa wazuri zaidi baadaye. Tunafanyia kazi hilo.”

Arsenal haijatazama nyuma tangu ilipofungwa kwa mara ya mwisho na Chelsea kwenye Ligi Kuu England, mechi zilizofuatia baada ya hapo, wote waliokumbana na timu hiyo kilichowapata kawaulize watakusimulia.

Kwa kasi hiyo ya Arsenal kwa sasa, Chelsea na Manchester City ambazo ndizo ziliifunga Arsenal kwenye mechi mbili za mwanzo za msimu huu, wakati Emery akiwa hajazoeana vyema na kikosi chake, hakika zitakuwa zimewekwa kiporo na wakikutana kwenye mechi za raundi ya pili, basi wajipange.

Juzi Jumapili, Washika Bunduki hao wa Emirates, walipiga mtu Bao Tano, huku mastaa wake matata, Alexandre Lacazette na Pierre-Emerick Aubameyang kila mmoja walitupia mara mbili, huku Aaron Ramsey akifunga bao bora la wikiendi kwenye Ligi Kuu England.

Hiyo ilikuwa kwenye mechi dhidi ya Fulham tena wakiwa kwao huko Craven Cottage.

Timu nyingine zilizokutana na fyekeo la Arsenal kwenye Ligi Kuu England msimu huu na kilichowapata ni balaa, Cardiff City alipigwa 3-2, Newcastle United 2-1, Everton 2-0, Watford 2-0, West Ham United 3-1 na Fulham waliopigwa 5-1. Kwenye michuano mingine, huko kwenye Europa League, Arsenal iliichapa Vorskla 4-2 na Qarabag 3-0, huku kwenye Kombe la Ligi, iliichapa Brentford 3-1. Kitu kinachotisha kuhusu Arsenal ya msimu huu inafunga mabao yanayoanzia mbili kwenda juu.

Kocha Emery amepiga mkwara kuwa wataendelea tu kugawa dozi kwa wapinzani wao watakaomenyana nao kwa kadiri inavyowezekana.

Advertisement