Huyu hapa mrithi wa Mourinho Manchester United

Sunday September 30 2018

 

JOSE Mourinho amekuwa akiisababishia Manchester United matatizo tangu mwanzo wa msimu huu ulipoanza. Kwanza alikuwa na ugomvi usiokwisha na winga Anthony Martial.

Hapo hujazungumzia yale malumbano yake na beki Luke Shaw na sasa kumekuwa na bifu kubwa baina yake na kiungo wa Kifaransa, Paul Pogba. Bifu hilo limedaiwa ni kubwa kiasi cha kuwafanya wachezaji wa Man United wagawanyike mara mbili huko kwenye vyumba vya kubadilishia, kundi moja likiwa upande wa Pogba na jingine upande wa Mourinho.

Hali hiyo imeelezwa kuwa mbaya kiasi cha Nemanja Matic na Juan Mata kugeuka kuwa wasuluhishi wa kuweka mambo sawa huko kwennye vyumba vya kubadilishia nguo. Wachambuzi wa mambo wanasema kwa hali ilipofikia kwa sasa, Mourinho anaweza asiwe na uhai tena kwenye kikosi hicho na kwamba muda wowote atafutwa kazi, kinachosubiriwa ni matokeo tu ya uwanja, ambapo jana Jumamosi walikuwa na mechi dhidi ya West Ham na kupigwa mabao 3-1 na kuzidisha hasira kwa kila mtu.

Wakati mchakato huo wa kutaka kufahamu hatima ya Mourinho huko Man United ukiendelea, hii hapa ndio orodha ya makocha wanne ambao wanaweza kuchukua mikoba yake na kurekebisha mambo.

5.Arsene Wenger

Manchester United inaweza kufanya uamuzi utakaowashangaza wengi kwenye soka la Ligi Kuu England. Uamuzi huo ni ule wa kumfuta kazi Mourinho na kisha kumchukua Arsene Wenger kushika mikoba kwa sababu kwa sasa Mfaransa huyo hana kazi yoyote. Hivi karibuni, Wenger ametangaza bayana kwamba hajastaafu, hivyo akiletewa dili la kuinoa timu yoyote atachukua mikoba huku ripoti zaidi zikifichua kwamba ameshawaambia wasaidizi wake wajiweka tayari kwamba muda wowote wanaweza kupata dili hasa baada ya kuona mwenendo wa Mourinho huko Man United.

4.Laurent Blanc

Laurent Blanc amehusishwa na Manchester United mara kadhaa huko. Kocha huyo Mfaransa alipata mafanikio makubwa alipokuwa kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain huko Ufaransa aliposhinda mataji matatu ya ligi katika kipindi chake cha miaka mitatu aliyokuwa kwenye timu hiyo. Aliwahi kuinoa pia timu ya taifa ya Ufaransa. Kiuchezaji, Blanc aliwahi kuichezea Man United, hivyo atakuwa na ufahamu wa utamaduni wa timu hiyo japo kwa kiasi kidogo tofauti na ilivyo kwa Mourinho kwa sasa. Blanc ni kocha mkali ambaye anaweza kuja kuifanya Man United kutoka hapo ilipo kwa sasa na kucheza soka linaloeleweka.

3.Ryan Giggs

Ryan Giggs ni mmoja kati ya wanasoka mahiri duniani waliowahi kuibukia kwenye klabu hiyo ya Manchester United. Baada ya kustaafu soka kama mchezaji, Giggs aliweka wazi matamanio yake ya kuja kuwa kocha wa Man United siku moja. Aliwahi kuwa kocha wa muda katika kikosi hicho wakati Man United ilipomfuta kazi David Moyes, aliyekuwa amepewa kazi kipindi ambacho Sir Alex Ferguson aliachana na timu hiyo. Faida kubwa ya Giggs ni kwamba ni mtu anayefahamu utamaduni halisi wa Man United, hivyo anaweza kuundeleza kama klabu kubwa zinavyofanya kuwa nafasi za ukocha wachezaji wao wa zamani.

2.Zinedine Zidane

Kutokana na kile alichokifanya akiwa na Real Madrid, Zinedine Zidane anatajwa kuwa kocha mwafaka wa kuja kuitoa Manchester United hapa ilipo na kuiweka kwenye makali yake. Man United chini ya Mourinho kwa sasa imeshindwa kabisa kuwa na kitu cha kutisha ndani ya uwanja kiasi cha kuzifanya timu maadui kutokuwa na kitu cha kuogopa wanapokabiliana na timu hiyo. Zidane alibeba mataji matatu mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya alipokuwa na Real Madrid, hivyo anaaminika kwamba anaweza kuja kufanya mambo makubwa zaidi Old Trafford. Zidane mwenyewe anaitaka kazi hiyo.

1.Mauricio Pochettino

Taarifa za kutoka kwenye magazeti mbalimbali ya Ulaya yanamhusisha kocha wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino na mpango wa kwenda kujiunga na Manchester United. Kocha huyo Muargentina ameripotiwa kwamba hata yeye mwenyewe anaonekana kuitaka kazi hiyo kubwa kabisa kwenye kazi ya ukocha. Pochettino amekuwa akifanya vyema huko kwenye kikosi cha Spurs na anapewa nafasi kubwa ya kwenda kufanya vyema kama akitua Old Trafford. Atakuwa chaguo bora kama atafuatwa kupewa kazi ya kumrithi Mourinho.

Advertisement