Tulieni! Sanchez mbona mtampenda msimu ujao

MANCHESTER, ENGLAND

SUPASTAA Alexis Sanchez amepanga kukatisha likizo yake na kurudi mazoezi mapema ili kujiweka fiti asije akafunguliwa mlango wa kutokea mapema bila ya kufanya mambo makubwa kwenye kikosi hicho.

Sanchez amekiri kuteswa na kiwango chake kibovu tangu alipotua Man United na mwishoni mwa msimu aliwaomba radhi mashabiki wa timu hiyo akidai majeraha yamemwangusha na kutibua mipango yake.

Staa huyo wa zamani wa Arsenal amefunga mara moja tu kwenye Ligi Kuu England msimu uliomalizika hivi karibuni na hivyo anataka kuanza mazoezi mapema sana ili kujiweka fiti akirudi msimu ujao aje kuwashika.

Alikuwa akiwekwa benchi tu chini ya Jose Mourinho kabla ya kuja kukutana na wakati mgumu tena mbele ya kocha mpya, Ole Gunnar Solskjaer.

Kulikuwa na taarifa kwamba angeondoka Old Trafford katika dirisha hili la majira ya kiangazi ili kuondokana na majanga ya soka la England.

Sanchez kwa sasa amerudi kwao Chile kusalimia familia na marafiki zake, mahali ambako atakuwa bize kufanya mazoezi ili kujiweka sana huku akitaka kurudi Carrington mapema zaidi kabla ya Julai 2, ambapo mastaa wengi wa Man United wameamua wawasili mazoezini kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.

Lakini, Sanchez amepanga kurudi mwishoni mwa Juni akianza kuingia kwenye mazoezi ya gym kujiweka fiti, Huko kwenye kikosi cha Man United, Sanchez analipwa Pauni 505,000 kwa wiki, lakini sasa anasakwa na Juventus na Inter Milan.