Msikie Aubameyang, kampa maujanja kibao Emery

LONDON, ENGLAND, SUPASTAA wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang amesema anaamini kwenye nafasi ambayo anacheza soka lake bora akipangwa mshambuliaji wa kati na si winga kama anavyofanya kocha Unai Emery.

Maneno hayo ya Aubameyang yanaelezwa kuwa ni ujumbe kwa kocha Emery kama anataka kufaidi mambo yake matamu zaidi basi anapaswa kumpanga kama straika na si winga.

Arsenal walikumbana na kichapo kwenye mechi yao iliyopita ya Ligi Kuu England walipomenyana na Manchester City na kuwafanya sasa waporomoke hadi kwenye nafasi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kufungwa mabao 3-1.

Aubameyang alizungumzia nafasi yake kwenye kikosi cha Arsenal akisema anajiona anakuwa bora zaidi akicheza straika na pembeni huku akidai anapenda zaidi kama atacheza na pacha kwenye fowadi hiyo ya Arsenal, ikiwa ni meseji kwa kocha Emery kwamba anapaswa kubadili fomesheni yake na kutumia 4-4-2 ili apange washambuliaji wawili kwa pamoja kama anavyotaka supastaa huyo wa kimataifa wa Gabon.

“Nafasi yangu ninayopenda kucheza ni straika, pale mbele. Napenda pia kucheza pembeni, lakini kwenye eneo ambalo nadhanni nakuwa bora zaidi ni straika,” alisema Aubameyang. “Napenda tucheze wawili mbele. Ni jambo zuri kwa sababu jambo hilo linakufanya utengeneze kombinesheni nzuri na mshambuliaji mwenzako. Lakini, ndiyo hiyo kama kocha atahitaji kucheza kulia au kushoto, hakuna namna. Nitacheza na nitajituma kwa ajili ya timu, hakuna shida.”