Mmemsikia Pogba? Kasema haondoki

Friday March 15 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND,

PAUL Pogba amewaambia Manchester United hana mpango wa kuihama timu hiyo baada ya kudai kwa sasa yupo kwenye furaha tele ya kuitumikia timu baada ya kuonyesha kiwango bora katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Kiungo huyo Mfaransa amekuwa kwenye kiwango bora kabisa tangu Man United ilipoanza kuwa chini ya Ole Gunnar Solskjaer baada ya Jose Mourinho kufutwa kazi Desemba mwaka jana.

Wakati wa Mourinho, Pogba alivurugwa na kwenye akili yake kitu kilichokuwa kimejijenga ni kuachana na timu hiyo huku Juventus alipokuwa ikitajwa kuwa kwenye mpango wa kutaka kumrudisha kwenye kikosi chake.

Lakini baada ya Mourinho kuondoka staa huyo wa Les Bleus amebadili msimamo wake na amekuwa na uhusiano mzuri na kocha wa sasa Solskjaer, ambaye wamekuwa wakizungumza mambo yao mara kwa mara.

Kilichopo, msimu ujao Pogba anaweza kutajwa kuwa nahodha wa timu hiyo wakati kipindi cha Mourinho alivuliwa hadi unahodha msaidizi katika kikosi hicho. Chanzo cha kutoka huko Old Trafford kilifichua: “Pogba amemwambia Ole hana mpango wa kuhama. Wamekuwa na mazungumzo marefu sana. Akili yake sasa imekaa sawa baada ya kupita kwenye kipindi kile cha majaribu kutoka kwa Mourinho. Sasa mchezaji huyo hauzwi kwa pesa yoyote ile na hilo lipo wazi, Pogba atabaki klabuni na haendi kokote.”

Man United inakabiliwa na vita nyingine kali ya kumtuliza kipa wake namba moja, David De Gea.

Advertisement