Makocha walipokutana na wachezaji wao wa zamani

Muktasari:

  • Kwenye maisha ya soka kuna wachezaji na makocha lakini pia mchezaji naye atafikia kiwango cha kustaafu kucheza mpira na kuwa kocha kama ana kipaji cha ukufunzi hili limebainika kwa baadhi ya wachezaji waliofuzwa na makocha wao wa zamani kukutana nao wakiwa kama wakufunzi rasmi na kuonyesha ubabe wao.
  • Huko  Ligi Kuu Scotland Brendan Rodgers na mchezaji wake wa zamani Steven Gerrard wakichuana kuwania ubingwa wa ligi hiyo, Rodgers akiwa kocha  na Celtic na Gerrard ni kocha wa Rangers.

LONDON ENGLAND.HUKO Ligi Kuu Scotland kuna mtu na mchezaji wake, Brendan Rodgers na Steven Gerrard wakichuana kuwania ubingwa wa ligi hiyo, Rodgers akiwa na Celtic na Gerrard ni kocha wa Rangers.

Huko England, siku si nyingi zimepita Manchester United walitupwa nje ya Kombe la Ligi baada ya kuchapwa na Derby County.

Lakini, kwenye mechi hiyo, kocha alipigwa na mchezaji wake wa zamani. Jose Mourinho, ambaye kwa sasa ni kocha wa Man United alichapwa na Derby, ambayo inanolewa na mchezaji wake wa zamani, Frank Lampard, ambaye alikuwa naye huko Chelsea.

Hata hivyo, hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa wachezaji kukutana na makocha wao za zamani baada ya hao pia kuwa makocha kutokana na kushuhudia mara kadhaa makocha wakikutana na wachezaji wao wa zamani. Cheki hapa kilichotokea mara nyingine 11 wakati wachezaji walipokutana na makocha wao wa zamani.

Steve Bruce vs Sir Alex Ferguson

Steve Bruce alikuwa gwiji kwenye beki ya Manchester United chini ya Kocha Sir Alex Ferguson. Ukabaji wake wa kibabe na uongozi wake mahiri ulimfanya kuwa nahodha shupavu katika kikosi hicho. Lakini, baada ya kuwa kocha, alikumbana na Ferguson kwenye mechi na mara zote, hakuwahi kumshinda. Wawili hao wamekutana mara 18 na mara nne tu ndio ilikuwa sare, huku 14 zote zikiwa vichapo kwa Bruce.

MauricioPochettino vs Marcelo Bielsa

Kuna hadithi nzuri kati ya Marcelo Bielsa na Mauricio Pochettino. Bielsa alimsajili Pochettino huko kwenye klabu ya Newell’s. Baadaye alimwita Muargentina huyo kwenye kikosi cha Argentina, wakati Bielsa alipokuwa kocha. Lakini, baada ya zama hizo kupita, wawili hao wote wakiwa makocha wamewahi kukutana mara tatu, wakati Pochettino akiwa Espanyol ilipomenyana na Athletic Bilbao ya Bielsa. Hapo, Pochettino alishinda mechi moja na kuchapwa mbili hivyo kuwa na rekodi ambayo imeshindwa kumpiku kocha wake wa zamani. Hapo ilidhihirisha kwamba mtoto kwa baba hakui.

Roberto Martinez

vs Kenny Jackett

Roberto Martinez sehemu kubwa ya uchezaji wake alikuwa kwenye kikosi cha Swansea City kilichokuwa chini ya kocha Kenny Jackett. Wawili hao hawakuwa wakielewana kabisa na Jackett alimweka sana benchi Martinez. Lakini, baadaye wawili hao wakakutana wote wakiwa makocha na Martinez alikuwa akiinoa Swansea na Jackett alikuwa Millwall kwa wakati huo. Mechi hiyo, mwalimu alimchapa mwanafundi wake. Lakini, mwaka 2013 wakati Martinez akiwa kocha Wigan, alikwenda kuichapa Millwall ya Jackett kwenye nusu fainali ya Kombe la FA, msimu ambao Wigan ilikwenda kubeba taji hilo. Wawili hao walikutana kwenye mechi mbili tu na kila mmoja ameshinda mara moja.

Mark Hughes

vs Sir Alex Ferguson

Mark Hughes enzi zake za uchezaji alikuwa mfungaji mahiri na mfungaji wa mabao mahiri. Yote hayo yalifanywa na Mark Hughes, ambaye alikuwa straika wa nyakati za mwanzo mwanzo za kocha Sir Alex Ferguson kwenye klabu ya Manchester United. Lakini, baada ya miaka kadhaa, wote wakawa makocha na wakakutana kwenye mechi za timu zao. Hughes na Ferguson wamekutana kwenye mechi 15 na nne zikimalizika kwa sare. Lakini, kwenye mechi hizo, Hughes ameshinda mbili tu na tisa alikumbana na kipigo kutoka kwa kocha wake wa zamani. Kwa Ferguson, Hughes mwana alibaki kuwa mwana.

Claude Puel

vs Arsene Wenger

Hii inachanganya zaidi kwa sababu Arsene Wenger anaonekana kijana na Claude Puel anaonekana mzee, lakini ukweli ni kwamba Wenger alimnoa Puel huko AS Monaco. Lakini, wote baada ya kuwa makocha, walikutana mara tano kwenye mechi za timu zao. Kwenye mechi hizo, mwalimu hawezi kushindwa na mwanafundi wake na ndio maana Wenger ameshinda mara tatu na mwanafunzi wake ameshinda mara mbili. Lakini, Puel ndiye aliyekuwa kocha wa kwanza kumfunga Wenger kwenye Kombe la FA kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu wakati walipokutana mwaka jana. Hawajawahi kutoka sare.

Pep Guardiola

vs Juanma Lillo

Pep Guardiola aliwahi kuwa chini ya kocha, Juanma Lillo. Lillo ndiye alikuwa mwanzilishi wa fomesheni ya 4-2-3-1 na Guardiola hata akaendelea kucheza huko Mexico ili mradi tu awe chini ya kocha Lillo. Lakini, baada ya Guardiola kuwa kocha akachuana na Almeria, timu iliyokuwa chini ya kocha wake wa zamani, Lillo. Wawili hao walikutana mara mbili, Guardiola akashinda mechi moja na nyingine ilimalizika kwa sare. Mhispaniola huyo ambaye ni kocha wa Manchester City kwa sasa, hakupoteza mechi yoyote wakati mara ya kwanza alipokutana na kocha wake wa zamani.

Phillip Cocu

vs Louis van Gaal

Phillip Cocu alikuwa gwiji wa PSV Eindhoven, ambaye kocha Louis van Gaal alimsajili akacheze Barcelona. Cocu alikwenda kufanya vizuri sana huko Nou Camp na alimkosha sana kocha wake. Muongo mmoja baadaye, Cocu akawa kocha wa PSV na timu yake ilikwenda kuchuana na Manchester United iliyokuwa chini ya Van Gaal kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Cocu akamchapa kocha wake wa zamani kwenye mechi ya kwanza iliyofanyika Eindhoven kabla ya kwenda kutoka sare Old Trafford. Wamekutana kwenye mechi mbili tu, Van Gaal amepigwa na mchezaji wake wa zamani moja na sare moja.

Diego Simeone

vs Gregorio Manzano

Diego Simeone amekuwa na mapenzi makubwa na Atletico Madrid. Katika miaka yake ya mwishomwisho ya kiuchezaji alirudi kwenye klabu hiyo na kubeba ubingwa katikati ya miaka ya tisini. Kipindi hicho kocha alikuwa Gregorio Manzano. Miaka kadhaa mbele, Simeone akawa kocha wa Atletico Madrid na Manzano alikuwa kocha wa Real Mallorca, wakakutana. Ilikuwa mechi ngumu kwa sababu mmoja alihitaji ushindi ili asishuke daraja. Wawili hao wamekutana mara moja tu na mechi hiyo ilimalizika kwa sare.

Carlo Ancelotti

vs Fabio Capello

Fabio Capello alichukua kiti cha ukocha AC Milan, kipindi hicho Carlo Ancelotti akiwa mchezaji. Kikosi chake kilikumbwa na majeruhi wengi na hivyo Capello, akaamua kumwondoa Ancelotti kwenye sehemu ya kiungo na kumtumia Demitrio Albertini. Pengine jambo hilo lilimkera Ancelotti na kuamua kuwa na vita binafsi na Capello baada ya yeye pia kuwa kocha na amekuwa akilipiza kisasi kwenye mechi walizokutana. Wamekutana mara 22 na Capello ameshinda mara tatu tu. Ancelotti amemnyanyasi bosi wake wa zamani, ambapo katika mechi hizo ameshinda mara 10 na kutoka sare tisa huku Capello akishinda tatu tu.

Zinedine Zidane vs Carlo Ancelotti

Ni hivi, Ancelotti aliwahi kumnoa Zidane kwa kipindi cha miaka mitatu walipokuwa pamoja Juventus. Lakini, baadaye alikuja kukutana naye tena Real Madrid na safari hii alikuwa msaidizi wake kwenye benchi la ufundi. Hayawi hayawi yamekuwa, Zidane akawa kocha mkuu wa Real Madrid na kumenyana na Bayern Munich ya kocha Ancelotti kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hapo ikawa mchezaji amekumbana na kocha wake. Walikutana kwenye mechi mbili na zote, Zidane ameshinda. Ancelotti amemshindwa mwanaye.

Roy Keane vs

Sir Alex Ferguson

Kama kuna mchezaji ambaye alizaliwa kuwa kocha, basi hilo unaweza kusema kuhusu Roy Keane. Kama kuna mchezaji ambaye alionekana bayana angekuja kuwa kocha basi alikuwa Roy Keane wakati alipokuwa Manchester United. Kwa jinsi alivyokuwa akiwaongoza wenzake ndani ya uwanja kwa vitendo na kuwaelekeza, watu waliamini angekuja kuwa kocha mzuri. Lakini, mambo yamekuwa kinyume chake, Keane amekuwa kocha wa ovyo. Akiwa kocha amekutana na mwalimu wake wa zamani Ferguson mara mbili katika msimu wa 2007/08 na mechi zote, Keane alichapwa.