Liverpool wataka kumrudia Coutinho

Monday June 24 2019

 

LIVERPOOL, ENGLAND

LISEMWALO ni kwamba Liverpool wanapiga hesabu za kuangalia uwezekano wa kumrudisha kiungo wa Kibrazili, Philippe Coutinho kwenye chama lao dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

Staa huyo amekuwa na wakati mgumu huko Nou Camp na mashabiki wa Barcelona wamekuwa wakimzomea wakiona hafanyi vile wanavyotaka wao. Lakini, Coutinho alikuwa na kipindi kizuri alipokuwa Liverpool, akifunga mabao 54 katika mechi 201 alizocheza akitokea kwenye kiungo kati ya mwaka 2013 na 2018 kabla ya kutimkia zake Barcelona Januari mwaka jana.

Huko Barcelona, Coutinho ameshinda taji la La Liga kwa misimu miwili mfululizo, lakini huduma yake ya ndani ya uwanja si tamu sana, akiwa amechangia mabao matano tu kwenye ligi kwa msimu uliopita. Kwa sasa staa huyo yupo na kikosi cha Brazil huko kwenye Copa America na hivi karibuni alisema anajiandaa kuachana na Barcelona.

Paris Saint-Germain wamekuwa wakihusishwa na mpango wa kumnasa fundi huyo wa mpira na mkurugenzi wa michezo mpya wa timu hiyo, Leonardo alisema klabu inafanya mchakati wa kulikamilisha dili hilo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Le 10 Sport, Liverpool nao wanamtaka staa wao wa zamani arudi Anfield kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi. Coutinho ameripotiwa kuwagomea Manchester United kwa sababu ya heshima kwa Liverpool.

Advertisement

Advertisement