Kuna mtu anamharibia Wenger ugali wake

Friday February 8 2019

 

PARIS, UFARANSA, BOSI aliyekuwa akiimiliki Olympique Marseille, Bernard Tapie amewapa onyo Paris Saint-Germain juu ya mpango wa kutaka kumpa kazi kocha Arsene Wenger.

Tapie amewaambia PSG kwamba wasithubutu kabisa kumpa kazi kocha huyo supastaa kwa sababu kitendo hicho kitakwenda kumweka kwenye wakati mgumu kocha wao wa sasa, Thomas Tuchel na mambo yataharibika.

Wenger amekuwa na urafiki wa karibu sana na rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi na jambo hilo limedaiwa linamfanya kocha huyo wa zamani wa Arsenal kufikiriwa kwenda kupewa kazi ya ukurugenzi wa michezo kwenye klabu hiyo yenye maskani yake Paris. Lakini, Tapie anaamini kumpa ajira mtu mwenye sifa na hadhi kubwa kwenye mchezo wa soka kama Wenger kutaondoa uwezo wa kujiamini wa kocha Thomas Tuchel kwa sababu atakuwa yupo chini ya supastaa wa soka.

“Hatawasaidia kitu kabisa. Kocha wao wa sasa ni mzuri. Kama wanadhani mkurugenzi hawaelewani, basi waajiri mwingine, lakini asiwe staa. Katika klabu, watu mnapaswa kuwa makini katika kuajiri watu mastaa kwenye nafasi kama hiyo muhimu.”

Advertisement