Kinda wa Liverpool ampa Van Dijk Ballon d’Or

Monday October 28 2019

 

LIVERPOOL, ENGLAND. KINDA wa Liverpool, Rhian Brewster anaamini kwamba Virgil van Dijk anastahili kushinda tuzo ya Ballon D’Or 2019, lakini amesema mpinzani mkali wa beki huyo kwenye tuzo hizo ni Roberto Firmino.

Kinda huyo ameanza kuibukia huko kwenye kikosi cha kwanza Anfield, lakini mwenyewe anafahamu ugumu unaomkabili katika kupata nafasi ya kucheza katika timu ya kwanza ya wababe hao wanaonolewa na Mjerumani, Jurgen Klopp.

Wachezaji saba wa Liverpool wameorodheshwa kwenye kinyang’anyiro hicho cha kusaka tuzo ya Ballon d’Or, ambapo Van Dijk na Firmino wameungana na Trent Alexander-Arnold, Alisson, Mohamed Salah, Sadio Mane na Georginio Wijnaldum.

Alipoulizwa nani atashinda tuzo hiyo, Brewster alisema beki Mdachi ndiye anayestahili baada ya kile alichokifanya na anachoendelea kukifanya kwenye kikosi hicho cha Merseyside.

“Kwanini beki wa kati asishinde Ballon d’Or?,” alisema Brewster.

“Watu watasema ameibadili Liverpool na hakika amekuwa akitusaidia kucheza mechi bila ya kuruhusu wavu wetu kuguswa. Nadhani Van Dijk atashinda.”

Advertisement

Van Dijk amepewa nafasi, lakini Brewster anaamini kama kuna mpinzani wa kumsumbua Mdachi huyo kwenye tuzo hiyo basi ni Firmino.

“Yupo kwenye tatu bora. Kama mshambuliaji, yupo pale kwenye orodha ya waliobora. Ni mchezaji mahiri kabisa, lakini hapewi tu thamani yake,” alisema kinda huyo na kuongeza: “Anaisaidia sana timu.”

Advertisement