Ishu ya Pochettino, Zidane yazua utata

Friday February 8 2019

 

LONDON, ENGLAND, MAURICIO Pochettino, David Beckham na Zinedine Zidane wamezidi kuibua utata baada ya watu hao watatu kuonekana wakienda kupata chakula cha usiku kwenye mgahawa mmoja huko London kabla ya kuondoka mmojammoja wakipitia mlango wauani.

Watu hao watatu ambao wana majina makubwa kwenye soka, walionekana kwenye mgahawa wa kibosi, Locanda Locatelli na walipoondoka, hawakuongozana, walitoka mmoja mmoja wakitofautiana kwa dakika tatu tu.

Zidane alikuwa wa kwanza kuondoka akipitia mlango wa jikoni na kutokea uwani, kisha akafuatia Beckham na baadaye Pochettino huku wakiwa wametofautiana kwa dakika tatu tu. Jambo hilo limezua utata mkubwa juu ya watu hao watatu.

Kocha wa Tottenham, Pochettino na Zidane wote wanahusishwa na kibarua cha kwenda kuinoa Manchester United mwishoni mwa msimu huu baada ya timu hiyo kuachana na Jose Mourinho.

Lakini, Pochettino anasakwa pia na Real Madrid, mahali ambako Beckham na Zidane waliwahi kucheza pamoja kabla ya mmoja kuwa kocha huko na kuachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu uliopita. Kwenye mgahawa huo waliokwenda ni kwa rafiki yake Beckham, Dave Gardner. Pochettino aliandamana na kocha wake msaidizi, Jesus Perez na jambo hilo ndilo lililoibua zaidi utata. Beckham na Zidane, walikuwa wakicheza pamoja kwenye ile Galacticos huko Bernabeu, wamekuwa marafiki wazuri hadi sasa na wamekuwa na uhusiano mzuri na rais wa Los Blancos, Florentino Perez.

Advertisement