IMEFICHUKA: Mourinho na Mbappe wanaenda Real Madrid

Monday October 28 2019

 

MADRID, HISPANIA. KAMA unaamini maneno ya wapambe, basi amini kocha wa zamani wa Real Madrid, Jose Mourinho atarudi klabuni hapo muda si mrefu kuanzia sasa. Na hatarudi peke yake, atafuatana na staa wa PSG, Kylian Mbappe.

Msaidizi wa zamani wa kocha huyo Mreno, Luis Campos ambaye aliwahi kufanya kazi na Mourinho katika kikosi cha Real Madrid, amedai kocha huyo atarudi klabuni hapo ambapo aliondoka mwaka 2013 na atatishja kama njaa.

Campos amedai pia staa wa kimataifa wa Ufaransa, Kylian Mbappe naye ataishia kukipiga Santiago Bernabeu wakati huu akiendelea kuhusishwa na uhamisho wa bei mbaya kuelekea Hispania mwakani.

“Real Madrid ni kitu kizuri. Jose Mourinho ni kitu kizuri. Ukichanganya vitu viwili vizuri unapata matokeo bora. Real Madrid inahitaji makocha bora na wasifu wa Mourinho unampa haki ya kufanya kazi na klabu bora,” alisema Compos.

Campos pia aliupigia debe uhamisho wa Mbappe kwenda Santiago Bernabeu baada ya kinda huyo mwenye umri wa miaka 20 kuingia uwanjani katika pambano dhidi ya Brugge Ligi ya Mabingwa wa Ulaya katikati ya wiki iliyopita na kupiga hat-trick katika ushindi wa 5-0.

“Nadhani ataishia kucheza Real Madrid. Kama anataka kuwa mchezaji bora duniani inabidi aichezee Real Madrid. Nadhani watakutana na Mourinho klabuni hapo,” alisema Compos.

Advertisement

Mourinho amekuwa hana kazi tangu Desemba mwaka jana wakati alipofukuzwa na Manchester United huku nafasi yake ikichukuliwa na kocha wa sasa, Ole Gunnar Solskajer na mara kadhaa amekuwa akionekana katika televisheni katika uchambuzi wa mechi mbalimbali.

Inadaiwa tayari amekataa ofa mbalimbali za kurudi kufundisha huku ikidaiwa klabu za Sporting Lisbon ya Ureno na Borussia Dortmund ya Ujerumani zilimpa ofa mezani lakini amegoma kusaini mikataba yao.

Inasemekana kocha huyo anaamini kocha wa sasa wa Real Madrid, Zinedine Zidane atafukuzwa wakati wowote kuanzia sasa na tajiri wa timu hiyo, Florentino Perez kabla ya kibarua hicho kusogezwa kwake.

Zidane alionekana kupunguza presha ya kufukuzwa hivi karibuni lakini kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Real Mallorca hivi karibuni kimerudisha presha kwake na kocha huyo anaweza kukalia kuti kavu kama ataendelea kupata matokeo ya aina hiyo.

Hivi karibuni Mourinho alihusishwa tena na Lyon ya Ufaransa lakini Rais wa Lyon, Jean-Michael Aulas alithibitisha kocha huyo aliitosa ofa yao kwa sababu tayari akili yake ameielekeza katika klabu nyingine.

Alhamisi usiku Mourinho ambaye ametwaa mataji matatu ya Ligi Kuu ya England akiwa na Chelsea alikuwa uwanjani kutazama pambano la michuano ya Europa kati ya Arsenal dhidi ya Vitoria katika Uwanja wa Emirates ambapo Arsenal ilishinda mabao 3-2 na kumpa nafuu Kocha Unai Emery ambaye kwa siku za karibuni amekalia kiti cha moto.

Mourinho pia amekuwa akihusishwa na wapinzani wa Arsenal, Tottenham ambao mambo hayawaendei vizuri kwa sasa huku Kocha Mauricio Pochettino akionekana kukalia kuti kavu. Hata hivyo, kocha huyo amefanikiwa kupunguza presha baada ya wiki iliyopita kuichapa Red Star Belgrade mabao 5-0 katika pambano la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Kwa upande wa Mbappe inadaiwa Rais wa Madrid, Florentino Perez ni shabiki mkubwa wa staa huyo wa zamani wa Monaco ambaye anamuona kama mchezaji Galactico aliyebaki sokoni anayeweza kunyanyua hadhi ya Madrid.

Mbappe amewahi kuhojiwa mara kadhaa na kushindwa kuthibitisha kama atabakia PSG kwa muda mrefu na inadaiwa hatasaini mkataba mpya klabuni hapo kwa ajili ya kuipa presha PSG imuuze kwenda Real Madrid katika dirisha kubwa la uhamisho lijalo la majira ya joto Juni mwakani.

Advertisement