Higuain atoswa Chelsea, arudishwa Juve

CHELSEA haina mpango wa kuongeza muda wa mkopo wa Gonzalo Higuain na itamrudisha klabu yake ya Juventus baada ya Fainali ya Europa League itakayopigwa Mei 29 dhidi ya Arsenal huko Baku katika dimba la Baku Olympic.

Higuain, 31, amefunga magoli matano tu katika mechi 21 tangu alipotua Stamford Bridge Januari mwaka huu kwa mkopo wa miezi sita.

Kuna kipengele cha kuongeza muda wake wa mkopo kwa msimu mwingine mmoja kwa ada ya Pauni 15.7 milioni au kumnunua jumla kwa Pauni 31.6 milioni.

Juventus hawamhitaji tena Higuain kwa sababu ana miaka miwili iliyobaki katika mkataba wake wa pesa ndefu, lakini idadi ya magoli aliyofunga kwenye Ligi Kuu ya England hairidhishi na kiwango chake kinafadhaisha.

Nafasi ya Higuain kwenye kikosi cha Juve kimejazwa na mkali wa kufumania nyavu Cristiano Ronaldo aliyebebwa kutoka Real Madrid.