He! Neymar ashikilia dili la Hazard Madrid

Friday February 8 2019

 

LONDON, ENGLAND, UMESIKIA hii? Ndoto za Eden Hazard kwenda zake Real Madrid huenda zikazimwa na supastaa wa Kibrazili, Neymar.

Mbelgiji huyo anayetajwa kuwa na thamani ya Pauni 100 milioni anaweza kuachana na maisha yake ya Stamford Bridge na matumaini yake ni kwenda kuichezea Los Blancos siku moja.

Shida inakuja sehemu moja tu, Real Madrid bado wanamtaka Neymar, ambaye anaweza kuwagharimu Pauni 200 milioni kutoka Paris Saint-Germain. Mbrazili, Neymar kwa sasa ameripotiwa kuwa na mpango wa kurudi tena kwenye La Liga na safari hii huenda akatua Bernabeu.

Mambo yalivyo ni kwamba kama Neymar atakubali kuondoka PSG, basi Hazard itabidi asuburi kwa sababu kinachoonekana ni kwamba atakuwa chaguo la pili kwenye mpango wa wababe hao wa Bernabeu.

Hazard kuhusu hatima yake huko Chelsea, alisema: “Nafahamu nitakachokwenda kufanya. Nimeshaamua.”

“Mnanifahamu nadhani, siku zote nimekuwa nikiipenda Real Madrid. Subiri tuone itakavyokuwa. Msimu huu nitamalizana na Chelsea. Bado nina mwaka mmoja katika mkataba wangu. Baada ya mwezi huu, tutajua.”

Hazard amekuwa na msimu mzuri kwenye kikosi cha The Blues akifunga mabao 12 na kuasisti mara 10 kwenye Ligi Kuu England.

Lakini, aliyesimama mbele yake ni Neymar, ambaye anaweza kutibua dili lake hilo kama PSG wanakuwa wepesi kuachana naye na kwenda kumchukua staa mwingine wa Chelsea, Mbrazili pia, Willian.

Advertisement