He! Bayern bana wanamtaka Klopp

Friday March 15 2019

 

MUNICH, UJERUMANI,

RAIS wa Heshima wa Bayern Munich, Franz Beckenbauer amesema atapenda kumwona Kocha Jurgen Klopp akijiunga kwenda kuinoa miamba hiyo ya Bundesliga siku moja.

Jambo hilo limeanza kuwatia presha Liverpool wakiwa na wasiwasi mkubwa huenda wakampoteza kocha wao huyo matata kabisa ambaye amewafikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati msimu uliopita aliwafikisha fainali na kuchapwa na Real Madrid.

Msimu huu, Klopp aliiongoza Liverpool kuiduwaza Bayern Munich nyumbni kwao kwa kuichapa 3-1 na hivyo kuwasukuma nje ya michuano hiyo na wababe wa Anfield wakihitimisha kuwa timu ya nne ya England kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo msimu huu.

Beckenbauer alisema: “Jurgen Klopp kuja FC Bayern? Hilo litakuwa jambo bora sana.

“Jurgen ni mtu aliyewafundisha Wajerumani namna ya kucheza soka lenye kasi.”

Mkataba wa Klopp huko Anfield utafika kikomo 2022 na mwenyewe amekiri amekuwa na furaha kubwa kwa kufanya kazi kwenye kikosi hicho ambacho pia kinafukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu kikichuana na Manchester City.

Advertisement