HII KALI: Mourinho adai hamjui Maurizio Sarri

Muktasari:

  • Ligi Kuu ya England limerudi Jumamosi mchana ni Chelsea dhidi ya Manchester United pale Stamford Bridge na kocha wa Manchester United, Jose Mourinho anarudi katika uwanja wake wa zamani Stamford Bridge ambao ulimpatia umaarufu mkubwa baada ya kutua England mwaka 2004 akitokea Porto ya Ureno.

LONDON, ENGLAND. MECHI za kimataifa zimepita na sasa joto la Ligi Kuu ya England limerudi vile vile. Jumamosi mchana ni Chelsea dhidi ya Manchester United pale Stamford Bridge na tayari vituko zimeanza kulizingira pambano hilo linalotazamiwa kuwa kali na la kusisimua.

Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho anarudi katika uwanja wake wa zamani Stamford Bridge ambao ulimpatia umaarufu mkubwa baada ya kutua England mwaka 2004 akitokea Porto ya Ureno. Safari hii anadai hamjui hata kidogo kocha wa timu yake ya zamani, Maurizio Sarri.

Sarri ambaye amekirithi kikosi cha kocha aliyetimuliwa, Antonio Conte kuanzia Julai 13 mwaka huu amefanya kazi kubwa ya kukisuka kwa haraka haraka kikosi hicho ambacho kilikuwa kimeparaganyika na tayari wameshinda mechi nane kati ya 12 katika michuano mbalimbali huku wakifunga mabao 22.

Kocha huyo Muitaliano hajawahi kukutana na Jose Mourinho katika pambano lolote la soka na Mourinho amekiri kwamba hamjui kocha huyo na wala hajawahi kukutana naye mahala popote.

“Simjui. Nilipokuwa Italia kuanzia mwaka 2008 hadi 2010 hakuwepo Serie A. sijawahi kukutana naye wala kucheza dhidi yake. Huwa namfuatilia tu katika soka na alifanya kazi nzuri wakati akiwa na Napoli.” Alisema Mourinho alipoulizwa kuhusu Sarri.

“England, makocha wote wazuri wana tamaa ya kuja. Kuna ushindani wa hali ya juu na kila kocha ana ndoto ya kuja kwahiyo alipata nafasi ya kuja. Ana timu nzuri sana, wachezaji wazuri na kikosi kizuri. Nadhani ana mazingira ya kufanya kazi nzuri,” aliongeza Mourinho.

Kwa upande wa Sarri amekuwa na hamu kubwa ya kukutana na Mourinho na msimu uliopita alikuwa na matumaini kwamba labda United ingepangwa na timu yake ya zamani Napoli katika pambano la Ligi ya mabingwa.

Kihistoria, Sarri alikuwa bado mfanyakazi wa benki wakati Mourinho akiingia katika kazi ya ukocha nchini Ureno na mpaka sasa Sarri bado hajafanikiwa kutwaa taji lolote la soka katika klabu nane za Italia ambazo amepitia.

Wakati Mourinho alipokuwa nchini Italia akichukua mataji matatu kwa mpigo na Inter Milan, Sarri alikuwa akifundisha klabu ya Serie B iitwayo Grosseto na alikuwa bado hajajitengenezea jina kubwa katika kazi ya ukocha kama ilivyo sasa.

Vinginevyo katika pambano la kesho presha kubwa ipo kwa kocha wa United, Mourinho ambaye alikaribia kufukuzwa kazi kabla ya mapumziko ya mechi ya kimataifa ambapo United walilazimika kupambana katika kipindi cha pili cha pambano dhidi ya Newcastle United baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0 na kisha kushinda mabao 3-2.

Mourinho ameiingiza United katika mwanzo mbaya zaidi katika historia yao ya Ligi Kuu ya England ndani ya miaka 29 baada ya timu hiyo awali kuambulia pointi 10 baada ya mechi saba kabla ya pambano hilo dhidi ya Newcastle.

Kwa upande wa Sarri, kikosi chake kinaongoza Ligi kwa pamoja na Manchester city na Liverpool ingawa City wapo kileleni zaidi kutokana na tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya wapinzani wao.

Kikwazo pekee kwa timu zote mbili huenda ukawa ni uchovu ambao utawakabili mastaa wa pande zote mbili ambao walisafiri maili nyingi kwenda katika mechi za kimataifa na timu zao za taifa katika mabara mbalimbali duniani kote kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita mpaka mwanzoni mwa wiki hii.