Duh! Bundesliga ngoma bado ngumu

MUNICH, UJERUMANI

UNAAMBIWA hivi, huko kwenye Bundesliga kumenoga kinoma baada ya bingwa wa msimu huu kusubiria hadi siku ya mwisho ya msimu ili kupatikana rasmi baada ya Bayern Munich kushindwa kupata matokeo dhidi ya RB Leipzig juzi Jumamosi.

Bayern inayonolewa na kocha Niko Kovac ilikuwa na nafasi ya kunyakua taji lao la saba mfululizo kwenye Bundesliga kama ingeshinda katika mechi hiyo, lakini sare ya bila kufungana imetibua kila kitu huku mahasimu wao Borussia Dortmund wakishinda mechi yao mbele ya Fortuna Dusseldorf na hivyo kufanya ubingwa kusubiri hadi mechi ya mwisho ya msimu itakayopigwa Jumamosi.

Timu hizo, Borussia Dortmund na Bayern sasa zimetofautiana pointi mbili tu kileleni kwenye msimamo wa Bundesliga, hivyo mambo yatasuburi hadi mechi za mwisho za msimu kupata bingwa. Hata hivyo, Bayern hawana presha kubwa sana kwa sababu sare tu kwenye mchezo wa mwisho utawapa nafasi ya kubeba taji hilo hata kama Dortmund watashinda mechi yao kutokana na wababe hao wa Allianz Arena kuwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa. Katika mechi za mwisho, Bayern watacheza na Frankfurt nyumbani, wakati Dortmund wanakabiliwa na Monchengladbach.