Benchi la Lukaku, Pogba lazua kizaazaa

Muktasari:

  • Kocha Jose Mourinho Jumatano  aliwaacha katika benchi mastaa wawili wa timu hiyo, Paul Pogba na Romelu Lukaku katika pambano dhidi ya Arsenal kwa kile alichoita sababu za mbinu na maarifa.

MANCHESTER, ENGLAND. Upepo bado haujatulia Old Trafford. Kila siku Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho anazua utata kutokana na maamuzi magumu ambayo anaendelea kuyafanya.

Baada ya United kuvurunda katika pambano dhidi ya Southampton wikiendi iliyopita, juzi Jumatano kocha huyo Mreno aliwaacha katika benchi mastaa wawili wa timu hiyo, Paul Pogba na Romelu Lukaku katika pambano dhidi ya Arsenal kwa kile alichoita sababu za mbinu na maarifa.

Mastaa hao waliingia kipindi cha pili cha pambano hilo lililomalizika kwa sare ya mabao 2-2 na kuiacha United ikiendelea kushika nafasi ya nane na kuongeza wasiwasi mkubwa wa kutoingia Top Four msimu huu.

Alipoulizwa kwanini aliwaacha Pogba na Lukaku katika benchi Mourinho alijibu: “Unajua, ni kwa sababu za kimbinu na kiufundi.

Tulienda kucheza na watu watatu, Lingard, Rashaford na Martial. Tuliwahi kufanya hivyo tayari huko nyuma na nadhani hivi karibuni dhidi ya Young Boys,” alisema Mourinho.

“Hatukufanikiwa kwa maana ya kufunga mabao lakini tulikuwa na furaha kwa jinsi tulivyotengeneza nafasi. Katika kipindi cha kwanza dhidi ya Young Boys hatukufunga lakini tulikuwa na nafasi kubwa.

Vijana wangu ni wadogo, Wako fasta, ni wachezaji wabunifu hata kama hauwezi kusema kama ni wamaliziaji wazuri,” alisema Mourinho.

Hata hivyo, staa wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka alionekana kutoafiki kitendo cha kocha huyo kuwaweka nje mastaa hao wawili ambao kwa pamoja thamani yao ni zaidi ya Pauni 160 milioni.

“Katika benchi naona United ina wachezaji bora. Ina benchi zuri sana. (Romelu) Lukaku, (Juan) Mata, (Paul) Pogba, (Marouane) Fellaini. Inashangaza sana. ndio amefaya mabadiliko na baada ya kuona kiwango dhidi ya Southampton wikiendi iliyopita nakubaliana naye,” alisema Rio na kuongeza: “Yalihitajika mabadiliko katika timu, hata hivyo, ni suala la kusubiri na kuona kama yana maana yoyote. Sikiliza kuna kitu inabidi kifanyike. Kitu cha kawaida ambacho tunakiona kila siku ni timu za Mourinho kubadilika wiki baada ya wiki.

Mabadiliko, mabadiliko, mabadiliko. Hata hivyo, hilo sio jambo jema kwangu kwa maana ya wachezaji na timu yenyewe. Unahitaji uhusiano mzuri ndani ya timu na hauwezi kubadilishana wachezaji kila wiki,” aliongeza Rio.

Staa mwingine wa zamani wa Manchester United, Paul Scholes ambaye mara nyingi amekuwa akicharurana na Mourinho alidai kocha huyo inabidi aishi vyema na Pogba kama ambavyo kocha wa Timu ya Taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps amekuwa akifanya.

“Namuangalia Paul Pogba wakati alipokuwa akiichezea Ufraansa katika Kombe la Dunia na jinsi alivyokuwa mchezaji muhimu.

“Hakuwa Pogba ambaye tumemzoea. Alikuwa Pogba mwenye madhara. Hii ilitokana na kuwa na kocha ambaye alimuwekea kanuni bora,” alisema Scholes.

Kauli ya Scholes inakuja wakati kukiwa na bifu linaloendelea kati ya Mourinho na staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa ambaye United ililipa dau la Pauni 89 milioni na kuvunja rekodi ya uhamisho ya dunia katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2016.

Inasemekana mara baada ya kumalizika kwa pambano dhidi ya Southampton wiki iliyopita, Mourinho alimwambia Pogba mbele ya wenzake alikuwa ni ‘kirusi’ ambacho kiliwaharibu wenzake na asingeweza kumvumilia.

Pogba amekuwa akikosoa mbinu za Mourinho za kucheza soka la kujihami zaidi na inadaiwa haridhishwi na hali hiyo na kuna uwezekano mkubwa uhusiano wao ukaendelea kudorora siku hadi siku.