Beki Pique atumika kumnasa Griezmann

Monday May 13 2019

 

BARCELONA, HISPANIA

UMESIKIA hii? Barcelona wamempa kazi Gerard Pique kuhakikisha anamshawishi staa wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann anakwenda kujiunga na klabu hiyo ya Nou Camp msimu ujao.

Griezmann, ambaye ni staa wa kimataifa wa Ufaransa aligomea uhamisho wa kujiunga na Barcelona kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana, akitangaza uamuzi huo kupitia video maalumu iliyorushwa kwenye televisheni katika fainali za Kombe la Dunia 2018 zilizofanyika huko Russia.

Baada ya kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa aibu, Barcelona wanaripotiwa kumrudisha Griezmann kwenye mipango yao ya kumnasa ili aende kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho. Barcelona wamedaiwa kuwa na uhakika wa kumnasa mtu wao katika dirisha lijalo la usajili na hivyo kumpa Pique kazi ya kuzungumza na mshambuliaji huyo ili ajiunge kwao.

Barca wanaamini watampata Griezmann baada ya kuthibitika kwamba Diego Godin, moja ya sababu zilizomfanya fowadi huyo asihame Atletico mwaka jana, ataondoka mwisho wa msimu huu baada ya mkataba wake kufika tamati.

Advertisement