Bata la Paul Pogba usipime unaambiwa

Monday June 24 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND

MAISHA yanahitaji nini tena kwa Paul Pogba. Anaishi kwenye jumba la Pauni 2.9 milioni. Ana ndege yake maarufu na ndinga za kifahari kama zote, zikiwa na thamani ya Pauni 1.6 milioni.

Si unajua hata saini yake Manchester United waliinasa kwa pesa nyingi mwaka 2016? Pauni 89 milioni, iliyoweka rekodi ya dunia kwenye uhamisho kwa kipindi hicho. Pogba anaishi anavyotaka.

Kwanza anasafiri kwa ndege yake mwenyewe na hivi karibuni baada ya msimu kumalizika alikwenda sake huko Perth, Singapore na Shanghai, ambako alikuwa bize kutangaza brandi yake ya PP.

Ni maarufu kweli kweli. Kwenye Instagram ana wafuasi 35 milioni, kwa wiki analipwa Pauni 290,000 na ndio maana anamiliki magari na kuishi maisha anavyopenda.

Baadhi ya magari anayomiliki Pogba ni Lamborghini Aventador, Rolls-Royce, Ferrari 812 Superfast na Chevrolet, Bentley, Audi RS6, Maserati Quattroporte na Mercedes GLS 4x4.

Advertisement

Baada ya kuishi kwenye hoteli ya Lowry kwa miezi sita, hatimaye, Pogba alipata makali yake mwenyewe, akimiliki jumba la kisasa kabisa lenye vyumba vitano vya kulala, ambalo thamani yake inatajwa kuwa ni Pauni 2.9 milioni.

Pogba ana kila kitu, hadi mitoko yake anayofanya si ya kitoto. Anafurahia maisha na mpenzi wake, mrembo Maria Zulay Salaues, ambaye ni mama wa mtoto wake mmoja. Tangu Kombe la Dunia 2018, Pogba amekuwa akila raha na mrembo huyo akifurahia maisha yake kama vile hakuna kesho.

Kwenye mitoko yake ya kwenda kula bata, Pogba amekuwa akipendelea zaidi kwenda zake Miami, Marekani, ambako kuna starehe kama zote hivyo, huku mara chache sana amekuwa akienda zake Dubai.

Kwa sasa jina lake linahusishwa zaidi na mpango wa kuondoka Man United, lakini jambo hilo halimfanyi kukosa fursa ya kufurahia maisha yake, akila bata tu kabla ya kipindi hiki cha mapumziko kumalizika na kurudi tena kwenye mchakamchaka wa msimu mpya wa ligi za Ulaya.

Advertisement