Aubameyang, Firmino sukuma ndani huko PSG

PARIS, UFARANSA

KOCHA wa Paris Saint-Germain, Thomas Tuchel amewataja nyota wake anaowataka kuwanasa kwenye dirisha hili la usajili na habari mbaya kwa Liverpool na Arsenal ni kwamba Roberto Firmino na Pierre-Emerick Aubameyang wapo kwenye mpango wake.

PSG ina kundi kubwa la wachezaji wenye vipaji vikubwa kama vile Neymar, Kylian Mbappe na Edinson Cavani, lakini wanataka kuwaongeza Firmino na Aubameyang kwenye orodha hiyo ili kuwanyoosha wapinzani wao msimu ujao.

Wameanza pia mazungumzo na Mbappe kwa ajili ya kumpa mkataba mpya, lakini ripoti zinadai Neymar na Cavani wanaweza kuchukua virago vyao na kuondoka kwenye timu hiyo mwishoni mwa msimu huu.

Hakuna ubishi Arsenal na Liverpool hazitakuwa tayari kuwaachia washambuliaji wake hao.

Firmino alitua Liverpool akitokea Hoffenheim mwaka 2015 na Aprili mwaka jana alisaini dili jipya la miaka mitano kudumu huko Anfield, wakati Aubameyang ndiyo kwanza hata mwaka mmoja na nusu hajafikisha kwenye kikosi cha Arsenal.

Msimu huu amefunga mabao 22 kwenye Ligi Kuu England na kushea Kiatu cha Dhahabu sambamba na mastaa wa Liverpool, Mohamed Salah na Sadio Mane, ambao pia kila mmoja amefunga mara 22.

Kuhusu Aubameyang, PSG inakabiliwa na vita kali kutoka kwa Real Madrid, ambayo pia inamtaka mchezaji huyo na tayari imetengwa Pauni 74 milioni kwa ajili ya kumnasa.