Waamuzi wa FIFA kuchezesha Mashemeji Derby

Saturday July 21 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Hatimaye ile mechi babkubwa ya mashemeji imefika mwanangu. Kesho kuanzia saa tisa alasiri, Gor Mahia na AFC Leopards watajitosa ugani Kasarani kukipiga kinoma noma. Waamuzi wa mtanange washajulika, halafu wana beji ya FIFA mazee!
Ndio, kuelekea mechi ya kesho, Shirikisho la soka nchini (FKF), imemteua Mwamuzi Israel Mpaima kutoka Narok, mwenye beji ya FIFA kuamua mbabe kati ya Ingwe inayonolewa na Muargentina Radolfo Zapata na Kogalo ya Muingereza Dylan Kerr.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mpaima atasaidiwa na Gilbert Cheruiyot na Jane Cherono kutoka Eldama Ravine na Mombasa mtawalia, mwamuzi wa mezani akiwa ni Kamaku Peter Waweru kutoka Aberdares, huku kamisa wa mchezo huo mkali akiwa ni mwamuzi mkongwe, Maxim Itur kutoka Nairobi.
Mchezo wa kesho ambao ni mechi ya kiporo namba 17, ambayo ilipaswa kupigwa Mwezi Mei katika uwanja wa Bukhungu Mjini Kakamega, lakini Shirikisho la Soka nchini liliamua kuuahirisha kupisha wachezaji kujiunga na timu ya taifa Harambee Stars ambao walikuwa na kibarua cha kuwakilisha taifa kimataifa.
Hii itakuwa mechi ya tatu inayowakutanisha miamba hawa wenye uhasimu mkubwa katika historia ya soka la Kenya msimu huu, ambapo rekodi inaonesha kuwa Gor Mahia wana kiburi cha kuibuka wababe baada ya kushinda mechi mbili zilizopita.
Kogalo wanaongoza msimamo wakiwa na pointi 49 huku Ingwe wakishika nafasi ya tano, wakiwa na pointi 37.

Advertisement