Simba, Yanga, Gor Mahia zapewa vibonde Sportpesa Super Cup

Monday May 28 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba pamoja na Gor Mahia, Yanga zimepewa vibonde katika mashindano Kombe la Sportpesa Super Cup yatakayoanza Juni 3 mjini Nakuru, Kenya.
Simba imepangwa kuanza na Kariobangi Sharks wakati mabingwa watetezi wa Kombe la Sportpesa Super Cup, Gor Mahia wataikabili Jeshi la kujenga Uchumi (JKU) ya Zanzibar mechi zitakazochezwa Juni 04, kwenye Uwanja wa Afraha, mjini Nakuru.
Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo inayodhaminiwa na Sportpesa, ikishirikisha klabu nane wanazodhaminiwa na kampuni hiyo, Mabingwa wa 27 wa Tanzania Bara, Yanga wenye watacheza Juni 3 dhidi ya Kakamega Homeboyz.
Miamba mingine Kenya, AFC Leopards watakuwa na shughuli pevu dhidi ya Singida United ya Tanzania (Juni 5) kwenye Uwanja wa Afraha.
Juni 6 itakuwa ni mapunziko kabla ya mashindano hayo kuendelea kwa hatua ya nusu fainali itakayopigwa Juni 7 na 8 mwaka huu.
Mtanange wa fainali utapigwa Jumapili ya Juni 10, kuanzia saa tisa alasiri. Kabla ya mechi hiyo, kutakuwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu utakaorindima kuanzia saa sita mchana.
Bingwa wa makala ya pili ya Sportpesa Super Cup, atakunja kitita cha shilingi 3milioni za Kenya (sawa Sh60 milioni) pamoja na kombe bila kusahau fursa ya kusafiri hadi Goodison Park, nchini Uingereza kujipima ubavu na klabu ya Everton.

Advertisement