Serikali yajitoa lawamani, masaibu ya timu ya Riadha ya Kenya, huko Nigeria.

Muktasari:

  • Ni kwamba, msafara wa wanariadha 64, walioondoka nchini siku ya Jumatatu, Julai 30, wakitumia ndege ya shirika la ndege la Kenya KQ 532, walijikuta wakikwama katika uwanja wa ndege Jijini Lagos, kwa takribani masaa 48, kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni kukosa ndege ya kuunganisha safari kutoka Lagos hadi Assaba.

Nairobi, Kenya. Serikali ya Kenya kupitia Wizara ya michezo jana jioni ilitoa ufafanuzi kuhusu masaibu yaliyoikumba timu ya Riadha ya Kenya, iliyoko nchini Nigeria kwa ajili ya kushiriki mashindano ya mbio za Shirikisho la Afrika, yaliyoanza jana huko Asaba Nigeria.

Ni kwamba, msafara wa wanariadha 64, walioondoka nchini siku ya Jumatatu, Julai 30, wakitumia ndege ya shirika la ndege la Kenya KQ 532, walijikuta wakikwama katika uwanja wa ndege Jijini Lagos, kwa takribani masaa 48, kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni kukosa ndege ya kuunganisha safari kutoka Lagos hadi Assaba.

Katika ufafanuzi na utetezi wao kuhusu tukio hilo, lililoikosesha Kenya ushindi kwenye mbio za mita 10,000, serikali ilijiondoa lawamani na kueleza kuwa tangu siku ya kwanza, imekuwa sambamba na kikosi hicho na kwamba wanafuatilia kwa ukaribu kilichosababisha kadhia hiyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi mtendaji mkuu wa michezo nchini, Hassan Noor, serikali imekuwa ikifuatilia swala hilo, hatua kwa hatua na kwamba tatizo lilianza na maandalizi mabovu ya safari, yaliyofanywa na kamati ya maandalizi ya mashindano hayo.

Kadhia hiyo, ilipelekea timu ya Kenya, kufika Asaba wakiwa wamechelewa kiasi cha kushindwa kufanya vizuri kwenye mbio za mita 10,000, ambapo mwanariadha Vincent Kipsang alimaliza katika nafasi ya nne, akitumia muda wa dakika 29, sekunde 14.52. Mshindi alikuwa ni Jemal Mekonnen wa Ethiopia.