Rais Kenyatta awaongoza Wakenya kumlilia Mama Oliech.

Muktasari:

Mama Mary Auma Oliech, alikutwa umauti akiwa nyumbani kwake Lavington, Jijini Nairobi, kwa mujibu wa mdogo wa Dennis Oliech aitwaye, Nickson Oliech.

Nairobi. Wingu zito la uzuni na simanzi limeendelea kutanga katika anga la michezo nchini Kenya kufuatia kifo cha Mama ya Straika wa zamani wa Harambee Stars, Dennis Oliech aliyefariki Dunia, jana Ijumaa, Julai 20, baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Mama Mary Auma Oliech, alikutwa umauti akiwa nyumbani kwake Lavington, Jijini Nairobi, kwa mujibu wa mdogo wa Dennis Oliech aitwaye, Nickson Oliech.
Miaka ya hivi karibuni hayajakuwa rahisi kwa mwenda zake, kutokana na maradhi ya saratani ambayo kwa kiasi kikubwa inadaiwa kuchangia kushuka kwa kiwango cha Dennis Oliech uwanjani.
Kutokana na mapenzi yake kwa Mama yake, wakati akiwa anaitumikia klabu ya St Etienne ya Ufaransa, itakumbukwa kwamba Oliech alilazimika kujipa mapumziko ya lazima kwa ajili ya kumuuguza mamake ambaye alikuwa amelazwa katika hospitali moja Jijini Paris. Baada ya hapo, straika huyo alijikuta akiishiwa pesa.
Unakumbuka namna ambavyo baadhi ya watu walivyoanza kumshambulia straika huyo anayetajwa kuwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi ambao wamewahi kutandaza kabumbu katika ardhi ya Kenya, akiwa Mkenya wa kwanza kucheza Ulaya? Naam yote hayo yalitokana na maradhi mamake.
Tuachane na hayo kidogo. Baada ya taarifa za kifo cha Mama Mary Auma kuripotiwa jana, wakenya nchini kote waliungana kumuombea na kutuma salamu za pole kwa familia ya Dennis Oliech wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, Waziri mkuu wa zamani, Raila Odinga na Rais wa Shirikisho la Soka nchini (FKF), Nick Mwendwa.
Katika salamu zake, kupitia ukurasa wa Twitter, Rais Uhuru Kenyatta alisema: Nimesikita sana kupata taarifa za kifo cha Mama Oliech, hii ni pigo kwa umma wa soka, pole sana familia na shujaa wetu Dennis Oliech, naelewa kwa sasa mnapitia wakati mgumu, kifo cha Mama Mary Auma kimetuacha na majonzi makubwa sana. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.
Kiongozi wa upinzani na Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga aliandika: Kwa majonzi makubwa sana nimepokea habari za kifo cha Mama yetu, Dada yetu na kipenzi chetu Mama Mary Auma. Huu ni msiba mzito kwa taifa na wapenzi wa soka. Mama Oliech atakumbukwa sana. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.
Naye Nick Mwendwa alisema: "Kwa niaba yangu na umma wote wa wapenda soka na wanamichezo nchini, napenda kuchukua nafasi hii kutoa pole zangu za dhati kwa Dennis 'The Menace' Oliech na familia yake kwa kumpoteza Mama yake mzazi. Sala zetu ziko nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Kwa upande wao, klabu ya Mathare United, ambapo ndugu watatu katika familia ya Mama Oliech ambao ni Dennis, Kevin na Andrew waliwahi kuitumikia kwa mafanikio makubwa, walitumia ukurasa wao wa twitter kutuma salamu zao za Rambirambi:
"Tunatuma rambirambi zetu za dhati kwa familia ya Mama Oliech. Dennis, Andrew na Kevin poleni sana kwa msiba huu. Tunamuomba Mungu awape moyo wa uvumilivu katika wakati huu mgumu, watabaki kuwa katika mioyo na sala zetu."