Mashabiki Gor wafungasha mabegi kujiandaa safari ya Goodison Parks

Friday June 8 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Wamepania kweli kweli. Kwani unadhani wanaambilika? Aah wapi, wameshafungasha mabegi, akili zao zinawatuma kukwea pipa kwenda Goodison Park, kwao wanaamini ubingwa ni wao na hakuna haja ya kutumia nguvu nyingi.
Mashabiki wa Gor Mahia buana, ni watu wa ajabu kweli kweli. Baada ya kuing'oa Singida United kwa mabao mawili ya Meddie Kagere, mashabiki wa Kogalo wakiongozwa na shabiki nambari wani wa klabu hiyo, Jaro Soja wanaamini shughuli imeisha!
Tovuti ya Mwanaspoti iliingia mtaani kusikiliza tambo za mashabiki wa klabu hiyo inayoongoza kwa mafanikio katika ukanda huu, unajua walisema nini kuhusu wapinzani wao Simba? Eti ni walaini sana.
Ndio, madhabiki wa Gor Mahia wanaichukulia poa klabu ya Simba. Wakichonga na Mwanaspoti mashabiki kindakindaki wa Kogalo Jaro Soja, Yvonne Akinyi, Joram Ochieng, Danny Silva wanaamini kikwazo pekee kilichokuwa mbele yao ni Singida United na hasa Kipa wa klabu hiyo Peter Manyika jnr.
Kwa mujibu wa Jaro Soja, mechi ya fainali itakuwa ngumu sana tofauti na inavyodhaniwa, lakini kivyovyote vile lazima Simba afe. Alisema baada ya kuwatazama mabingwa hao wa ligi kuu ya Vodacom, amegundua wanafungika kirahisi, kinachotakiwa ni Meddie Kagere kuwa katika hali nzuri kimchezo.
"Game itakuwa ngumu, Simba wako poa, lakini sioni wakitusumbua kama Singida. Tumeshajiandaa kwenda England, hapo tunapita tu fasta. Tuombe Mungu Kagere akue fiti," alisema Jaro.
Kwa upande wake, Danny Silva aliwamwagia sifa mabingwa hao watetezi wa Sportpesa Super Cup na kwa mujibu wa kauli yake mwenyewe, kupitia ukarasa wake wa Facebook, alisema kama klabu hiyo ingekuwa ndio timu ya taifa, Kenya ingekuwa Kombe la dunia na kumalia, Goodison Park tunakuja.
Hata hivyo, wakati mashabiki hao wakitoa tambo zao kuelekea mchezo wa fainali utakaopigwa siku ya jumapili, Juni 10, katika uwanja wa Afraha mjini Nakuru, Kocha wa klabu ya Gor Mahia, Mwingereza Dylan Kerr, anaamini tofauti.
Akizungumza na kituo kimoja cha habari cha humu nchini, Kerr alionesha kuihofia Simba ambayo alipata kuinoa miaka kadhaa ya nyuma na kusisitiza kuwa mchezo huo utakuwa mkali kuliko mechi ya nusu fainali.
Gor Mahia walijikatia tiketi ya kwenda fainali kwa kuifungisha virago klabu ya Singida United, kwa ushindi wa mabao 2-0, katika mechi ya nusu fainali ya pili. Kwa upande wao Simba walifuzu kwa kuiong'oa Kakamega Homeboyz kwa mikwaju ya penalti. Simba ilishinda 5-4.

Advertisement