Kenya yatikisa kwa medali Jumuiya ya Madola

Saturday April 14 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Wanariadha Elijah Manangoi (mita 1500) na Hellen Obiri (mita 5000), wameongeza tabasamu katika nyuso za Wakenya baada ya kuongeza medali mbili za dhahabu katika kapu la medali la taifa hilo.

Manangoi alitumia dakika 3:34.78 na kunyakuwa medali ya dhahabu akimshinda Mkenya mwenzake, Timothy Cheruiyot aliyetumia dakika 3:35.17 na kushinda medali fedha.

Nafasi ya tatu ilienda kwa Jake Wightman, kutoka Scotland akitumia dakika 3:35.97 katika makala ya 21 ya mashindano hayo yaliyoingia siku ya 10 leo, Jijini Gold Coast, Australia.

Awali mwanadada, Hellen Obiri aliipatia Kenya medali yake ya tatu ya dhahabu baada ya kushinda mbio za mita 5000, akitumia dakika15:13.11kuvuka utepe huku nafasi ya pili ikienda kwa mkenya mwenzake, Margaret Kipkemboi aliyetumia dakika 15:15.28.

Nafasi ya tatu ilienda kwa Muingereza Laura Weightman (15:25.84) akimaliza sekunde mbili mbele ya Mganda, Juliet Chekwel (15:30.17). Mkenya mwengine katika mbio hizo, Eva Cheroni alimaliza katika nafasi ya saba.

Ushindi wa Obiri, Manangoi, Cheruiyot na Kipkemboi unaifanya Kenya kufikisha jumla ya medali 17 ambazo ni dhahabu 4, fedha 7 na shaba 6 na kukaa katika nafasi ya 13 kwenye jedwali la mashindano hayo.

Medali za dhahabu kwa Kenya mpaka sasa zimepatikana kupitia kwa wanariadha Wycliffe Kinyamal (mita 3000 viunzi), Conseslus Kipruto (mita 3000 viunzi na maji), Hellen Obiri (mita 5000) na Elijah Manangoi (mita 1500).