Kenya yatinga fainali Intercontinental Cup

Friday June 8 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Timu ya taifa ya Kenya, 'Harambee Stars' imefanikiwa kutinga fainali ya michuano ya Hero Intercontinental Cup, inayoendelea nchini India, baada ya kuicharaza Chinese Taipei mabao 4-0, katika mchezo mkali uliomalizika muda mfupi uliopita, katika uwanja wa Mumbai Football Arena.
Katika mchezo huo mkali, beki wa Posta Rangers, Jockins Atudo, alizama wavuni mara mbili huku Nahodha wa Thika United, Dennis Odhiambo na Straika wa Tusker FC, Timothy Otieno, wakitupia goli moja kila mmoja.
Kikosi cha Stars kinachonolewa na Sebastien Migne, kitakutana na wenyeji India katika fainalo, wakiwa na lengo la kulipiza kisasi kwani itakumbukwa kuwa katika mechi ya pili ya makundi, wahindi hao waliipiga Stars 3-0.
Harambee Stars walikuwa wanahitaji ushindi wa mabao yasiyopungua magoli matatu, kutinga fainali na hii ni baada ya New Zealand kuinyuka India 2-1, katika mechi kali iliyopigwa jana. Mechi ya fainali itapigwa siku ya Jumapili, Juni 10.
Kikosi cha Harambee Stars:
Patrick Matasi, Jockins Atudo, Erick Ouma, Michael Kibwage, Musa Mohamed, Duncan Otieno, Dennis Odhiambo, Cliff Miheso, Patillah Omoto, Ovella Ochieng, Pistone Vunyoli.
Akiba: Timothy Odhiambo (Kipa), Vincent Wasambo, Timothy Otieno, Johnstone Omurwa, Bernard Oginga, Crispin Oduor, Kenneth Muguna, John Makwatta and Bolton Omwenga.

Advertisement