Migne aanza kwa kipigo

Friday May 25 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Kocha wa Harambee Stars ya Kenya, Mfaransa Sebastien Migne ameanza vibaya baada ya kikosi chake kuchapwa bao 1-0, na Swaziland katika mchezo wa kirafiki uliomalizika muda mchache uliopita.
Katika mchezo huo mkali uliopigwa Uwanja wa Kenyatta, Mjini Machakos, Kenya watajilaumu wenyewe baada ya kupoteza nafasi nyingi za wazi huku safu yao ya ulinzi ikifanya makosa kadhaa ya hatari ambapo kama sio uimara wa mlinda lango, Boniface Oluoch, Kenya ingefungwa mabao mengi.
Katika dakika ya 78, straika hatari wa Swaziland, Barry Steenkamp, aliwatoka mabeki  wa Stars kirahisi na kuipatia timu yake bao pekee na ushindi. Barry, aliunganisha krosi nyepesi kutoka upande wa kulia wa uwanja, na kumfunga kirahisi, Bonface Oluoch.
Kipigo hiki, kinamfanya Sebastien Migne kuwa kocha wa tatu, kupoteza mchezo wake wa kwanza na timu ya taifa katika historia ya mchezo huo nchini. Wakufunzi wengine walioangukia katika mechi ya kwanza na Harambee Stars ni Bernard Lama na Henry Michel.
Kwa upande wao, Swaziland wana kila sababu ya kukenua kwani huu unakuwa ushindi wao wa kwanza dhidi ya Kenya ugenini katika miaka ya hivi karibuni.
Itakumbukwa kwamba mwaka 2000, Swaziland walikula kichapo cha 3-0 waliokutana na kikosi cha Stars kilichokuwa kikinolewa na James Siang'a. Miaka saba baadae wakafungwa 2-0 na vijana wa Jacob Mulee.
Kibarua kinachofuata kwa Kocha Migne na vijana wake, itakuwa ni dhidi ya Equatorial Guinea. Mechi hii ya kujipima nguvu itapigwa katika uwanja wa Machakos, Mei 28.

Advertisement